Dar es Salaam. “Machozi ya mama anayesubiri kurejeshewa mwili wa mwanae ni kilio kisicho na sauti, lakini chenye uzito mkubwa kwa taifa”.
Huo ndio ujumbe uliotolewa na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, akisisitiza kuwa “machozi ya mama ni deni la taifa” na kwamba Tanzania inahitaji uponyaji wa kweli kufuatia kilichotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata.
Chama hicho kupitia Ngome ya Wanawake leo Machi 3, 2026 kimezindua mnara wa kumbukumbu wa mashujaa waliopoteza maisha kufutia vurugu za Oktoba 29, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake.
Akizungumza na waandishi wa habari na wanachama wa chama hicho, Dorothy amesema taifa haliwezi kusonga mbele kwa amani ya kudumu bila kukabiliana kwa uwazi na ukweli kuhusu matukio yaliyoacha majonzi kwa familia nyingi.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Machi 3, 2026 wakati wa uzinduzi wa mnara wa kuwakumbuka Watanzania waliopoteza maisha kutokana na vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Tunalaani vikali ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa kwa Watanzania. Taifa linahitaji uponyaji, na uponyaji huo hauwezi kupatikana kwa kuficha ukweli au kupuuza kilio cha waathirika,” amesema.
Dorothy amesema hatua ya kwanza kuelekea haki ni kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi itakayokuwa nje ya Serikali, akidai kuwa tume iliyoundwa sasa haiwezi kuwatendea haki Watanzania kwa sababu ya kukosa uhuru wa kimuundo na kimamlaka.
“Tunahitaji tume ambayo haitapokea maagizo kutoka kwa mtu yeyote. Tunataka tume itakayoanza na kufanya tathmini ya kile kilichotokea, tunataka tume itakayopita na kuhakikisha watu wote waliohusisha wanawajibishwa bila kujali vyeo vyao.
“Kwa kuwa hakuna aliye juu ya sharia, tunataka walioshiriki katika kupanga, kutekeleza mauaji haya wawajibishwe, tunataka takwimu halisi halisi za waliopoteza maisha na kuhakikisha miili ya marehemu inakabidhiwa kwa familia zao ili waweze kupata mazishi ya heshima.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu pamoja na makada wa chama hicho wakati wakiweka mshumaa kwenye mnara wa kuwakumbuka Watanzania waliopoteza maisha kutokana na vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 uliozinduliwa leo Jumanne Machi 3, 2026 katika makao makuu ya chama hicho Magomeni.
Amesema bila uwajibikaji wa wazi na wa haki, majeraha ya kitaifa yataendelea kuota mizizi na kuathiri mshikamano wa kijamii.
“Heshima ya mwisho si zawadi, ni haki. Familia zinahitaji kufunga ukurasa kwa kuwapumzisha wapendwa wao kwa taratibu zinazostahili,” alisema.
Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na mjadala mpana kuhusu uwajibikaji, haki na maridhiano ya kitaifa, huku wadau wa siasa na asasi za kiraia wakisisitiza umuhimu wa kujenga imani ya wananchi kwa taasisi za dola.
Akizungumza kwenye tukio hilo, Mkuu wa Kanisa la Morovian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki askofu, Emmaus Mwamakula amesema lengo si kulipiza kisasi, bali kujenga taifa linalosimama juu ya haki, ukweli na utu.
“Tunachokitafuta si mgawanyiko, bali maridhiano ya kweli. Lakini, maridhiano hayawezi kujengwa juu ya maumivu yaliyofichwa. Lazima ukweli usemwe, haki itendeke, na walioumizwa wapate faraja.
Mnaondelea na mapambano msikate tamaa na msikubali kugawanywa. Hakuna mahali popote ambapo mapambano ya kudai haki yalipatikana kwa urahisi. Kilichotokea Oktoba 29 ni mbegu kuelekea kwenye ushindi,” amesema.
Mbali ya kuzindua mnara huo wanawake wa ACT Wazalendo wamejipanga kuwatembelea wanawake nchi nzima kuwahamasisha kuendelea kushiriki kwenye mapambano ya kudai demokrasia.