
Dar es Salaam. Mgogoro wa umiliki wa Ploti Namba 9 Ursino Estate, Msasani wilayani Kinondoni, uliokuwa ukimilikiwa na aliyekuwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Ernest Mashimba, umechukua sura mpya baada ya wakili wa Ally Rubeya, Stephen Mosha, kufafanua madai ya familia ya marehemu kuwa mteja wake alijitwalia ardhi hiyo kinyume cha sheria.
Hatua hiyo inakuja siku chache tangu wakili wa familia ya Mashimba, Peter Madeleka, kutoa siku 14 kuanzia Februari 22, 2026 kwa Rubeya kuachia eneo hilo, akidai hakuna mkataba halali unaomruhusu kuendelea kulitumia.
Akizungumza na waandishi wa habari, Wakili Mosha amesema mteja wake alinunua eneo hilo kihalali kutoka kwa mke wa marehemu aliyekuwa msimamizi wa mirathi, baada ya yeye mwenyewe kutangaza kuuza mali hiyo.
Amesema katika makubaliano ya mauziano, muuzaji aliweka sharti la kupatiwa nyumba mbili na viwanja viwili kwa ajili ya watoto wake, pamoja na fedha taslimu na gari.
Kwa mujibu wa Mosha, Rubeya alitoa nyumba mbili zilizopo Magomeni (Plot Na. 97 Block U na Plot Na. 24 Block T) zenye thamani ya Sh420 milioni, viwanja viwili Mbweni Mpiji vyenye thamani ya Sh50 milioni, gari aina ya Toyota Prado yenye thamani ya Sh50 milioni na fedha taslimu Sh280 milioni.
“Mauziano hayo yalifanyika kwa makubaliano ya pande zote, na nyaraka ziliandaliwa na wakili wa muuzaji,” amesema Mosha.
Mkataba wa miaka 99
Mosha amesema baada ya Rubeya kuanza mchakato wa kubadili umiliki wa hati, alielezwa kuwa hati hiyo ingeweza kuhamishwa baada ya miaka 25, hivyo kwa ushauri wa kisheria wakaingia makubaliano ya mkataba wa miaka 99 mwaka 2012.
Amesema mkataba huo ulisajiliwa Wizara ya Ardhi na kumpa Rubeya haki ya kuendelea kumiliki eneo hilo kama mpangaji wa muda mrefu.
“Baada ya mchakato kukamilika, msimamizi wa mirathi alisaini hati ya kukiri kutomsumbua mteja wangu,” amesema.
Ameongeza kuwa Rubeya alipohitaji kubomoa nyumba iliyokuwapo katika eneo hilo, aliomba kibali kupitia kwa muuzaji na kibali kilitolewa kwa jina lake, ndipo akaanza ujenzi.
Madai ya utapeli
Kwa upande wake, Madeleka amedai Rubeya aliingia kwenye makazi hayo kama mpangaji, lakini mwaka 2013 aliomba kibali cha kubomoa nyumba wakati suala la mirathi likiwa bado mahakamani.
Amesema mwaka 2021, baada ya mirathi kukamilika na watoto wa marehemu kuwa wamiliki halali, walishangaa kuitwa tena wasimamizi wa mirathi, hali iliyozua sintofahamu juu ya umiliki.
Madeleka amesisitiza kuwa msimamizi wa mirathi hana mamlaka ya kuuza mali ya urithi bila kufuata taratibu, na kwamba familia haitakwenda mahakamani bali inataka Serikali iingilie kati kumaliza mgogoro huo.
Hata hivyo, Mosha amepinga hoja hiyo akisema kisheria msimamizi wa mirathi anaweza kuuza mali ya marehemu kwa manufaa ya warithi.
Shauri mahakamani
Mosha amesema mwaka 2014 Rubeya alipatiwa notisi ya siku 14 kuondoka katika eneo hilo kupitia kampuni ya udalali ya Unyangala Auction Mart, hatua iliyomlazimu kufungua shauri la ardhi namba 75 ya mwaka 2015.
Amesema mahakama ilitoa zuio la kuondolewa kwa Rubeya katika eneo hilo na kuthibitisha haki yake ya kumiliki kwa mujibu wa mkataba wa muda mrefu.
Aidha, amedai muuzaji aliwahi kuripoti polisi Kituo cha Kawe akidai kuibiwa hati na kubomolewa nyumba bila kibali, lakini alishauriwa kutatua suala hilo kwa maridhiano kwa kuwa ni mgogoro wa kimkataba.
Mgogoro huo sasa unaendelea kuzua mjadala huku kila upande ukishikilia msimamo wake, wakati familia ya marehemu ikisisitiza kuwa ilitapeliwa, na Rubeya akidai alifuata taratibu zote za kisheria katika ununuzi wa eneo hilo.