
Wengi wetu, kufikiria maisha baada ya kifo ni jambo gumu. Hata hivyo, kufikiria ni muhimu sana kwa sababu maisha yanaweza kuwa mafupi na yasiyotabirika hata hivyo wosia ni moja ya mambo bora unayoweza kufanya wakati bado una afya na akili timamu ili kuhakikisha wapendwa wako wanapata usaidizi wa haki na mzuri endapo utakufa.
Katika mazingira ya kijamii na kisheria ya Tanzania, wosia si tu nyaraka ya kurithi mali ni njia ya kuweka amani, kuepuka migogoro na kulinda familia yako baada ya wewe kushindwa kuwasiliana nao tena.
Kwa Tanzania, sheria inayosimamia masuala ya urithi na usimamizi wa mali za marehemu ni sheria ya Uthibitisho wa wosia na usimamizi wa mirathi (Probate and Administration of Estates Act) ya mwaka 1963. Sheria hii inatoa mwongozo wa jinsi mali za mtu zitakavyogawanywa endapo atakufa akiwa na wosia au bila wosia.
Kwa mtu anayefariki bila wosia, mali zake hugawanywa kwa kutumia sheria za urithi za nchi. Hii mara nyingi ina maana kwamba mali inaenda kwa familia kwa mtiririko unaokubaliwa na sheria, na si lazima kwa mapenzi ya mtu aliyefariki.
Kuandika wosia kunakuwezesha kusema wazi unataka nini kitokee na mali zako kama nyumba, ardhi, gari, fedha benki au mali zingine za thamani baada ya kifo chako. Kwa mfano, unaweza kubainisha nani anastahili kupata ardhi yako au kutunza watoto wako wachanga endapo wao hawana mlezi mkubwa.
Hii ni njia ya kuhakikisha kwamba mapenzi yako yanaheshimiwa na kwamba wapendwa wako hawapotezi muda mwingi wa kubishana mbele ya mahakama au familia. Bila wosia, mara nyingi shughuli za kugawa mali zinachukua muda mrefu na kutumia pesa nyingi kwa mashauri ya mahakama, jambo ambalo linaweza kuwa mzigo kwa familia yako.
Kwa kuwa na wosia pia inasaidia kuzuia migogoro ya kifamilia. Watu wanaweza kuwa na matarajio tofauti kuhusu urithi, hasa pale mali ni nyingi au zenye thamani kubwa. Kuandika wosia kwa uwazi na kwa ushauri wa mwanasheria kunasaidia kupunguza migogoro hii kwa sababu mapenzi yako yamekwishaandikwa na kuthibitishwa mbele ya mashahidi, na si mawazo yanayobadilika baada ya kifo.
Sheria ya Tanzania inatoa mwafaka wa kisheria kwa wosia, lakini pia ina mambo maalum ya kufuata ili wosia uwe wa halali. Mtunzaji wa wosia lazima awe na uwezo wa kisheria yaani awe na umri wa miaka 18 au zaidi na akili timamu ili kuelewa kile anachofanya. Wosia ni lazima uweke taarifa za mali zako, jinsi zinavyogawanywa na nani unataka awe msimamizi.
Msimamizi huyu ndiye atakayeshughulikia ugawaji wa mali zako kwa kukutana na mahakama na kuhakikisha mapenzi yako yanafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria. Kwa mfano, kama wosia hauandikwi vema au kama hakuna msimamizi aliyeteuliwa, mahakama inaweza kuchukua muda mrefu kuamua nani atasimamia mali zako.
Ikumbukwe kuwa kuandika wosia sio tu kwa ajili ya mali, bali pia ni zawadi ya amani kwa familia yako. Inawasaidia kupambana na machungu ya msiba bila kuwa na wasiwasi mwingi wa masuala ya mali.
Kwa kuchukua hatua sasa, unaweka ushawishi mzuri wa maisha yako hata baada ya kifo, na kuhakikisha kuwa zile mali ulizojenga kwa nguvu yako zinaleta manufaa kwa wale unaowapenda na sio chanzo cha migogoro