
Wachambuzi wa masuala ya diplomasia wamesema mapigano yanayoendelea kati ya Iran, Israel na Marekani yameiweka njia panda Pakistan ambayo ni mshirika wa nchi mbili kati ya tatu zinazoshambuliana.
Februari 28 mwaka huu yalianza mashambulizi ya anga yaliyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran huku yenyewe ikijibu mapigo kwa Israel na kambi za kijeshi za Marekani katika ukanda huo.
Kutokana na Iran kuzilenga kambi za Marekani, imejikuta ikirusha makombora yake hadi katika mataifa mengine ya jirani ambayo hayahusiki moja kwa moja katika mzozo huo jambo ambalo limeifanya vita hiyo kuwa ya ukanda mzima.
Iran mbali na kuishambulia Israel pia inazilenga kambi za Marekani zilizo katika nchi za Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) huku mashambulizi yake pia yakitua Kuwait, Oman, Bahrain, Uturuki na Iraq.
Wakihojiwa na mitandao wa Dawn kwa masharti ya kutotajwa majina, wachambuzi hao wameishauri serikali ya Pakistan kuwa makini na mapigano hayo kwa madai kuwa huenda yakasababisha ipoteze ushirika wake na Marekani au Iran.
‘’Pakistan imekuwa na jukumu muhimu kwa kuipa Marekani kambi za mashambulizi ya hivi karibuni ya UAV dhidi ya Iran. Hapo awali ilishirikiana na Marekani na kutoa taarifa za kijasusi kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran,’’ walidai wachambuzi hao.
Wameeleza kuwa kuna baadhi ya mataifa kama Hispania yamekuwa na msimamo thabiti ili kutoingia katika mzozo na mataifa mengine.
‘’Pakistan, Saudi Arabia, Israel na Marekani wanapata manufaa binafsi kutokana na mzozo wa sasa huko Asia Magharibi. Pakistan inafaidika kiuchumi na itavuna ulinzi na neema za kisiasa kutoka Marekani na Saudi Arabia. Hilo lisiwe sababu ya kupoteza ushirika na mataifa mengine, umakini unahitajika,’’ wamedai.