Mwanza. Boti iliyokuwa imebeba abiria na mizigo imeteketea moto na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine 50 kuokolewa katika Ziwa Victoria ikitokea Kisiwa cha Gozba mkoani Kagera kuelekea Mwanza.

Akizungumza kwa simu, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Elisa Mugisha amesema waliopoteza maisha ni jinsia ya kiume ambao ni mtoto anayekadiriwa kuwa na miaka 10 pamoja na mtu mzima wa miaka 60.

Amesema ajali hiyo imetokea katikati ya kisiwa cha Lyamwenge na Bwiro vilivyopo Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza alfajiri ya leo Alhamisi Julai 9, 2026.

Amesema manusura hawana majeraha bali walipata mshtuko na kupelekwa hospitali ya Bwiro na wengine Lyamwenge kupata huduma ya kwanza.

“Boti hapa katikati imepata ajali ya kuungua kwa moto na mpaka muda huu (saa saba mchana)  tumeishaokoa watu 50…Bahati mbaya wawili wamepoteza maisha ni jinsia ya kiume.

“Mtoto anakadiriwa wa miaka 10 na mtu mzima wa miaka 60. Ila hao wengine waliokuwa na hali mbaya wamepelekwa hospitali kupata huduma,” amesema.

Mugisha ameongeza kuwa; ” Mpaka sasa hivi tunaendelea kuthibitisha je, walikuwa 52 tulioambiwa ili tukiweza kupata kumbukumbu rasmi tutakuwa tumesalia na watu wawili, lakini inawezekana kuna wengine labda walizidi kwa hiyo kinachoendelea sasa hivi ni kuthibitisha idadi iliyokuwepo na kwenda kuwatafuta wale wanaotajwa wawili ambao mpaka sasa hivi hatujawapata.”

Ameeleza boti hiyo imeteketea na moto kutokana na upepo mkali uliowazuia hata wao kufika kwa wakati eneo la tukio.

“Tukimaliza uokoaji tutaanza uchunguzi  wa kujua chanzo cha moto huo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *