
Mapema mwezi huu, jeshi la Suda Kusini (SSPDF) ilitangaza kuwa linapanga kufanya operesheni za kijeshi katika mji wa Akobo na vijiji vinavyozunguka, na kuwaelekeza raia kuondoka katika maeneo hayo kabla ya operesheni hizo kuanza.
Katika tangazo hilo la tarehe 6 Machi, 2026 jeshi hilo pia liliwataka walinda amani wa Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wa misaada ya kibinadamu kuondoka Akobo ndani ya saa 72.
Hata hivyo, UNMISS imesema itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa kitaifa, wa majimbo na wa ngazi za jamii ili kuhakikisha usalama wa raia katika eneo hilo.
“Operesheni zozote za kijeshi ndani au karibu na Akobo zinaweka hatarini sana usalama wa raia,” amesema Anita Kiki Gbeho, Afisa anayekaimu uongozi wa UNMISS. Ameongeza kuwa ujumbe huo unategemea ahadi za pande zote kwamba zitachukua hatua zote zinazowezekana kulinda jamii.
UNMISS imesisitiza kuwa walinda amani wake wataendelea kuwepo Akobo ili kutoa ulinzi kwa raia, hasa ikizingatiwa kuwa eneo hilo linahifadhi idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano.
Ujumbe huo pia umekumbusha kuwa usalama wa wafanyakazi wake, majengo na mali zake lazima uheshimiwe kikamilifu wakati wote.
