UONGOZI wa Simba unaangalia uwezekano wa kuipata saini ya beki wa kati raia wa Ivory Coast, Serge Anthony Badjo baada ya kutokuwa na uhakika zaidi juu ya hali ya afya za mabeki wawili, Abdulrazack Hamza na Wilson Nangu.

Simba inaangalia uwezekano huo wa kumpata Badjo mwenye miaka 23, ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na USM Khenchela aliyojiunga nayo Agosti 17, 2025, akitoka MC Algiers zote za Algeria kuisha tangu Juni 30, 2026.

Chanzo kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti uongozi wa timu hiyo hauna uhakika wa moja kwa moja juu ya mabeki wawili wa kikosi hicho, Abdulrazack Hamza na Wilson Nangu ikiwa watarejea mapema kutokana majeraha yao.

Hamza alifayiwa upasuaji wa goti tangu Desemba 2025 katika kliniki ya Zerktouni iliyopo jijini Casablanca nchini Morocco, ili kurekebisha jeraha alilopata akiwa na kikosi hicho kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Septemba 16, 2025.

Kwa upande wa Nangu, alifanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu Afrika Kusini Februari 18, 2026, baada ya beki huyo kupata jeraha katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia.

Kutokana na majeraha ya nyota hao wawili, uongozi wa Simba unaangalia uwezekano wa kuongeza beki mwingine wa kati na Badjo ni miongoni mwao, licha ya kufanya vizuri kwa mabeki wengine ambao ni Ismael Olivier Toure na Rushine De Reuck.

Chanzo kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti, licha ya afya ya Hamza na Nangu kuimarika siku baada ya siku, lakini bado kuna uwezekano wa kuchelewa kucheza kwa msimu ujao kutokana na kuhitaji muda zaidi.

“Toure na De Reuck wamefanya kazi kubwa sana lakini msimu ujao tuna mashindano mengi na tunahitaji kufanya vizuri zaidi ya msimu wa 2025-2026, ili kuendana na mahitaji yetu ni lazima tuongeze nguvu nafasi mbalimbali,” kilisema chanzo hicho.

Simba inaamini inaweza kumpata Badjo kwa sasa kwa sababu ni mchezaji huru na suala la kukubaliana maslahi binafsi sio ishu kubwa, huku uzoefu wake wa kucheza timu za Yopougon FC na SOL FC d’Abobo zote za kwao Ivory Coast ukichangia pia.

Hata hivyo, Simba italazimika kuangalia idadi ya wachezaji wa kimataifa ndani ya kikosi chake kwani katika msimu wa 2025-2026 ilikuwa nao 12 wanaotakiwa kikanuni, ili kusajili mchezaji mwingine wa kimataifa, haina budi kupunguza waliopo.

Miongoni mwa nyota wa kimataifa wanaotajwa huenda wasiwepo Simba kwa msimu ujao ni mshambuliaji Mghana, Jonathan Sowah aliyeingia kwenye mgogoro na klabu hiyo hali iliyopelekea kusimamishwa kabla ya kutakiwa kufanya mazoezi na timu ya vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *