UN: Zaidi ya watu wapya 100,000 Lebanon wakimbia makazi yao  ndani ya saa 24 sababu ya vitaUN: Zaidi ya watu wapya 100,000 Lebanon wakimbia makazi yao  ndani ya saa 24 sababu ya vita

Wimbi hili jipya la wakimbizi ni sehemu ya mgogoro wa kikanda ambao umeongezeka kwa kasi katika siku za hivi karibuni. 

Mashambulizi ya kijeshi yaliyoanzishwa tarehe 28 Februari na Israel pamoja na Marekani dhidi ya Iran, yakilenga vituo vya kijeshi na maghala ya mafuta nchini humo, yalichochea haraka mlolongo wa mashambulizi ya kulipiza kisasi na mvutano kote Mashariki ya Kati. 

Wakati Tehran ikitoa vitisho dhidi ya washirika wa Washington katika kanda hiyo, maeneo kadhaa ya mzozo yameanza kuwaka.

Mashambulizi yaongezeka Lebanon

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, jeshi la Israel limeongeza mashambulizi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na Hezbollah, kundi la kijeshi la Kishia linaloungwa mkono na Iran na ambalo ni mhusika muhimu katika siasa na jeshi la Lebanon. 

Mashambulizi ya kurushiana makombora katika mpaka wa Israel na Lebanon, ambayo hayakuwa yamekoma kabisa tangu vita vya mwaka 2024 kati ya Tel Aviv na Hezbollah, yameongezeka katika siku za karibuni na kulazimisha mamia ya maelfu ya wakazi kukimbia maeneo yanayoshambuliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kutoka Beirut leo Jumanne, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, nchini Lebanon, Karolina Lindholm Billing, amesema hadi sasa zaidi ya watu 667,000 nchini Lebanon wamejisajili kwenye mfumo wa mtandaoni wa serikali ya Lebanon kama watu waliokimbia makazi yao, ikiwa ni ongezeko la watu 100,000 katika siku moja tu.

Afisa huyo wa UNHCR amesisitiza kuwa idadi hiyo inaonesha “kasi kubwa zaidi ya watu kukimbia makazi yao” ikilinganishwa na kipindi cha vita vya mwaka 2024 kati ya Israel na Hezbollah.

Mwakilishi wa UNHCR na wafanyakazi wenzake wa DPNA wanasambaza misaada ya msingi kwa familia zilizohamishwa katika makao ya pamoja huko Adra, Saida Governorate, Lebanon. Wanaume wenye mavazi ya mkononi wanapakua misaada kutoka kwenye lori.

© UNHCR/Houssam Hariri

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakitoa misaada kwa familia zilizohamishwa makazi yao katika eneo la Sidon, kusini mwa Lebanon.

Makumi ya maelfu wakikimbilia Syria

Zaidi ya hayo, tangu tarehe 2 Machi, karibu Wasyria 80,000 pamoja na zaidi ya Walebanon 7,700 wamevuka mpaka kuelekea Syria wakikimbia mashambulizi ya mabomu.

“Miongoni mwao kuna wakimbizi wa Syria waliokuwa wakipanga kurejea nyumbani katika miezi ijayo, na wengine ambao wamelazimika kurudi haraka kutokana na kuongezeka kwa mapigano ya sasa,” ameeleza Karolina Lindholm Billing.

Kwa mujibu wa UNHCR, watu wanaowasili mpakani watoto, watu wazima na wazee mara nyingi wanaonesha dalili za mshtuko na hofu baada ya kukimbia maeneo yaliyoshambuliwa kwa mabomu.

Hatari ya milipuko ya magonjwa kwenye makazi ya wakimbizi

Kadri idadi ya watu wanaokimbia makazi yao inavyoongezeka, mashirika ya kibinadamu yanaanza kuhofia mgogoro wa afya. 

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) linaonya kwamba msongamano mkubwa katika makazi ya muda na vituo vya kupokea wakimbizi unaongeza sana hatari ya milipuko ya magonjwa.

“Moja ya wasiwasi wetu ni ugonjwa wa surua kwa watoto, lakini pia sasa kwa kuwa tuko katika majira ya baridi, tunaweza kuona maambukizi zaidi ya magonjwa ya njia ya kupumua,” amesema leo Jumanne Dkt. Abdinasir Abubakar, mwakilishi wa WHO nchini Lebanon, akizungumza kutoka Beirut.

Shirika hilo la afya sasa linaona hatari ya kuenea kwa magonjwa kutokana na harakati kubwa za watu kuongezeka. 

Shirika hilo linaboresha mifumo ya tahadhari na ufuatiliaji katika makazi ya wakimbizi na kujaribu kuharakisha chanjo kwa watoto waliokimbia makazi yao dhidi ya surua na magonjwa mengine yanayozuilika kwa chanjo.

Wakimbizi wa Afghanistan waliorudi kutoka Iran wanakusanyika kwenye mpaka wa Islam-Qala karibu na Herat na mizigo yao na mali zao. Watoto wapo miongoni mwa waliorudi. UNICEF inatoa misaada ya kibinadamu na huduma za ulinzi wa watoto katika dharura hii kali.

© UNICEF/Azizullah Karimi

Waafghanistan waliorudi kutoka Iran wanakusanyika kwenye mpaka wa Islam-Qala, karibu na Herat magharibi mwa Afghanistan.

Hospitali katika shinikizo, wahudumu wa afya wauawa

Kuongezeka kwa mapigano kunaleta shinikizo kubwa kwa mfumo wa afya wa Lebanon. 

Kwa mujibu wa WHO, hospitali na timu za dharura zinajitahidi kukabiliana na idadi kubwa ya majeruhi huku zikijaribu kuendelea kutoa huduma muhimu za matibabu.

Mashambulizi yaliyolenga huduma za afya tayari yamesababisha vifo vya wahudumu 14 wa huduma za dharura na wafanyakazi wengine wa afya, huku wengine 24 wakijeruhiwa. 

Kwa jumla, vituo 56 vya afya vimeathiriwa, hospitali tano sasa hazifanyi kazi, na hospitali nne zimeharibiwa kwa sehemu.

Shule zageuzwa makazi ya wakimbizi

Kote nchini, miundombinu ya kiraia sasa inatumiwa kuwahifadhi watu waliokimbia makazi yao. Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura (OCHA), shule 287 za umma sasa zinatumika kama makazi ya pamoja, hali inayowanyima karibu watoto 90,000 fursa ya kupata elimu.

Hali ni ngumu zaidi kwa wafanyakazi wahamiaji ambao ni wengi katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) linakadiria kuwa takriban wahamiaji 30,000 wako katika maeneo yaliyolengwa na mashambulizi ya mabomu au yaliyopewa amri ya kuhamishwa.

OCHa imeongeza kuwa “Wahamiaji waliotelekezwa na waajiri wao kusini wanasaidiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali na makundi ya kijamii kufika katika maeneo salama zaidi,” 

Imeongeza kuwa “upatikanaji wa wahamiaji kwenye makazi ya pamoja bado ni mdogo na juhudi zinaendelea kutafuta suluhisho mbadala la malazi.”

Sehemu katika Beirut, Lebanon inayoonyesha familia za wakimbizi wanaoishi mitaani. Mbele, mwanamume analala kwenye benchi, wakati mwanamke aliyevaa suti ya kijani na hijab ameketi karibu na mtoto katika gari. Vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hookah, vimetapakaa karibu nao. Watu wengine wanaonekana nyuma kwenye barabara ya jiji.

© UNICEF/Dar al-Mussawir

Wanafamilia wakipumzika barabarani mjini Beirut, Lebanon, baada ya kukimbia nyumba zao kutokana na amri ya kuhamishwa.

Mgogoro wa kibinadamu wenye athari za kikanda

Nchini Iran, mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya maghala ya mafuta yamesababisha kutolewa kwa kiasi kikubwa cha kemikali hatari angani.

Kwa mujibu wa WHO, mashambulizi hayo yanaweza kusababisha mvua yenye sumu katika baadhi ya maeneo ya Tehran. 

“Tunaendelea kuwasiliana na hospitali na mamlaka, na mamlaka za Iran zimetoa tahadhari kwa wananchi kubaki majumbani, hasa kutokana na mashambulizi dhidi ya maghala ya mafuta,” amesema Christian Lindmeier, msemaji wa shirika hilo.

Shirika hilo pia linafuatilia hatari za kiafya zinazotokana na “kutolewa kwa kiasi kikubwa cha kemikali za hidrokarboni zenye sumu, hewa ukaa yenye salfa na misombo ya nitrojeni angani.

Waafghani walazimika kurejea kutoka Iran

Athari za mgogoro wa kikanda pia zinaonekana mashariki zaidi mwa nchi hiyo. UNHCR inaripoti kuwa takriban Waafghani 110,000 wamerejea kutoka Iran tangu mwanzo wa mwaka huu, sawa na karibu watu 1,700 kwa siku.

Katika mpaka wa Iran na Afghanistan, timu za kibinadamu zina hofu kwamba kuongezeka kwa mapigano kutasababisha watu zaidi kulazimika kuhama.

“Watu niliokutana nao leo wamesema wameathiriwa moja kwa moja na mashambulizi ya mabomu na hawajihsi salama tena, huku wengine wakieleza kuwa kupanda kwa bei na shinikizo la kiuchumi kunafanya maisha yao kuwa magumu zaidi,” amesema Arafat Jamal, mwakilishi wa UNHCR nchini Afghanistan.

Kadiri mzozo kati ya Israel, Marekani na Iran unavyoendelea kutikisa kanda hiyo, wahudumu wa misaada ya kibinadamu wana hofu kwamba wimbi hili la watu kukimbia makazi yao linaweza kuwa ishara ya mwanzo wa mgogoro mkubwa zaidi ambao athari zake zinaweza kuenea mbali zaidi ya mipaka ya Lebanon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *