
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, katika mazungumzo ya simu na Rais wa Russia, amesisitiza ulazima wa kulaaniwa vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika majukwaa ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB), jioni ya Jumanne, mazungumzo ya simu yalifanyika kati ya Rais wa Russia Vladimir Putin, na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, kwa pendekezo la upande wa Russia.
Katika mazungumzo hayo, marais wawili wamejadili masuala muhimu yanayohusu ushirikiano wa pande mbili pamoja na matukio ya kikanda, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.
Rais wa Russia, amesisitiza tena msimamo wa nchi yake wa kupinga uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran, na ametangaza utayari wa nchi yake kutoa misaada inayohitajika pamoja na ushirikiano wowote utakaosaidia kumaliza haraka mivutano na mapigano katika eneo.
Kwa upande wake, Rais Pezeshkian ametoa shukrani kwa msimamo wa Russia katika kuunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na huku akiashiria uchokozi unaoendelea wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya miundombinu ya kiraia na raia wa kawaida ameseisitiza kwamba: “Kuna ulazima wa kulaaniwa kwa vitendo hivyo vya uchokozi na uhalifu wa Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni katika majukwaa ya kimataifa.
Marais wa nchi hizo mbili pia wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza mashauriano na mawasiliano katika ngazi za juu kati ya pande hizo mbili.