
Aston Villa imekuwa timu pekee ya Ligi Kuu England kupata ushindi katika mechi za mkondo wa kwanza wa hatua za mtoano za Mashindano tofauti ya Ulaya wiki hii.
Timu hiyo jana usiku imeibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Lille ya Ufaransa jana katika hatua ya mchujo ya mashindano ya Europa League.
Bao pekee la Aston Villa katika mchezo huo limefungwa na Ollie Watkins katika dakika ya 61 akimalizia pasi ya Emiliano Buendia.
Tofauti na Aston Villa, Nottingham Forest na Crystal Palace zimeshindwa kupata ushindi jambo ambalo limefanya timu nane tofauti za EPL kushindwa kupata ushindi katika mashindano ya Ulaya wiki hii.
Katika Europa League, Nottingham Forest jana imechapwa nyumbani kwa bao 1-0 na Midtyjylland huku Crystal Palace ikilazimishwa sare tasa nyumbani na AEK Larnaca katika Kombe la Conference League.
Kabla ya timu hizo, Jumatatu na Jumanne mambo yalionekana kuwa magumu kwa timu sita za EPL zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa zote kushindwa kupata ushindi katika mechi zao za mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora.
Liverpool ilichapwa bao 1-0 na Galatasaray, Manchester City ikafungwa mabao 3-0 na Real Madrid, Chelsea ikapoteza kwa mabao 5-2 mbele ya PSG, Tottenham Hotspur ikapoteza kwa mabao 5-2, Newcastle United ikatoka sare ya bao 1-1 na Barcelona na Arsenal ilimaliza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Bayer Leverkusen.