Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaka nchi za Kiislamu kuwa macho dhidi ya njama za maadui wa pamoja wa Umma wa Kiislamu.

Marais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Abdel Fattah al-Sisi wa Misri siku ya Ijumaa walibadilishana mawazo katika mazungumzo ya simu kuhusiana na matukio ya kieneo na kimataifa kufuatia hujuma za kijeshi za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.

Katika mazungumzo hayo, Pezeshkian amesema, Marekani na utawala wa Kizayuni zinatekeleza dhamira na malengo maovu ya kutaka kudhoofisha na kugawanya Iran na nchi nyingine kubwa za Kiislamu na kusisitiza kuwa: Marekani na Israel hazitavumilia kuwepo kwa nchi kubwa na zenye nguvu za Kiislamu kama vile Iran, Misri, Uturuki na Saudi Arabia katika eneo. Rais wa Iran amezitaka nchi za Kiislamu kuwa macho dhidi ya njama za maadui wa pamoja wa Umma wa Kiislamu na kusisitiza kuwa: “Nchi za Kiislamu hazipaswi kuruhusu Marekani na Israel zizue mifarakano baina ya nchi za Kiislamu kwa kuibua mifarakano.”

Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais wa Misri pia ameonya juu ya matokeo hatari ya kuendelea vita na migogoro dhidi ya uthabiti na usalama wa eneo na dunia, na kutoa wito wa pande zote husika kuwa na subira na kujiepusha kuongeza zaidi mivutano, na kueleza kuwa yuko tayari kufanya juhudi zozote kwa ajili ya kukomesha vita na kurejesha amani na usalama katika eneo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *