DAR ES SALAAM: SHEIKH Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Shia nchini, Hemed Jalala, ametoa wito kwa Waislamu duniani kote kuimarisha umoja ili kusimamia haki za watu, akisisitiza kuwa mshikamano ni muhimu kupinga dhuluma maeneo mbalimbali duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya ya kimataifa ya Quds, ambayo hufanyika kila Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jalala amesema umoja wa Waislamu ni msingi muhimu katika kulinda utu na haki za binadamu.

Amesema wito huo pia uliwahi kusisitizwa na aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Khamenei, ambaye mara nyingi amehimiza Waislamu kuwa kitu kimoja katika kusimamia haki za watu wanaodhulumiwa duniani.
“Moja ya malengo makubwa ni kuhakikisha Waislamu wanakuwa kitu kimoja katika kusimamia haki za wanaodhulumiwa duniani,” amesema Jalala.
Aidha, alikumbusha dunia kuwa amani na utulivu ni mambo muhimu kwa ustawi wa jamii, akionya kuwa vitendo vya dhuluma na kumwaga damu vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali vinaathiri ustawi wa binadamu.

Ametaja maeneo yanayokumbwa na migogoro ikiwemo Gaza, Palestine, Lebanon na Iraq, akisema hali hiyo inaonesha namna dhuluma ilivyoendelea kutawala katika baadhi ya sehemu za dunia.
“Tunawakumbusha walimwengu kuwa dhuluma ni kitu kinachopaswa kuondolewa, huku tukihimiza kuenzi utu, umoja wa Waislamu na umoja wa kitaifa,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa maadhimisho ya International Quds Day yanatoa fursa kwa Waislamu na jamii kwa ujumla kukumbushana umuhimu wa kusimamia haki, amani na mshikamano wa watu duniani.
Kwa upande wake,Mkuu wa Chuo Cha Jamia Al Mustafa International Sayyid Arif Naqvi amesema wanafahamu kuwa wanaoteseka zaidi katika migogoro hiyo ni watoto na wanawake.
“Tumekusanyika hapa kupigania haki yao ili waweze kuishi kwa amani kama binadamu wengine,” amesema.