KIGOMA; MKUU wa Mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro ameongoza viongozi wa serikali na mamia ya wananchi wa Mkoa Kigoma kuaga miili ya watumishi 7 wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma waliofariki kwa kuzama na boti Ziwa Tanganyika jana, huku vilio vikitawala wakati wa kuaga miili hiyo.
Akizungumza wakati wa kuaga miili hiyo, Balozi Sirro alisema kuwa marehemu wanaagwa wakiwa mashujaa, kwani wamekufa wakitekeleza majukumu ya kitaifa na kwamba ni simanzi kubwa kupoteza idadi kubwa ya watumishi, huku wengine wakiwa ndiyo wanaanza taratibu za utumishi.

Amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amechukua jukumu lote la a kugharamia masanduku ya kusafirishia miili hiyo, pia rambi rambi ya Sh milioni moja kwa kila mwili na shilingi 200,000 kwa kila majeruhi na kwamba gharama za matibabu zote zitalipwa na serikali hata ikilazimika kupata rufa kwenye hospitali kubwa nchini.
Miili ya watumishi waliagwa ni Erick Dabanga (27), Jofrey Aron (26), Rachael Msalila (29), Winny Bayabusani (32), Joyce Kandole (31), Paul Luvanda (31) na Omari Karim (29) na hadi sasa mwili wa Amos Sika haujapatikana.