Katika ufunguzi wa Mkutano huo afisa mwandamizi wa UNODC ameonya kuwa ulaghai wa kifedha umegeuka kuwa moja ya uhalifu unaokua kwa kasi zaidi duniani, ukichochewa na maendeleo ya teknolojia na mitandao ya uhalifu ya kimataifa.

Afisa huyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC John Brandolino ametoa onyo hilo wakati akiwakaribisha washiriki wa mkutano huo, wakiwemo mawaziri, viongozi wa kampuni za teknolojia, taasisi za fedha, wanazuoni na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Polisi wa makosa ya Jinai INTERPOL,  na pia unaadhimisha miaka kumi ya ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili katika kupambana na uhalifu wa kimataifa wa kupangwa.

“Kuleta pamoja sauti na mitazamo mingi kiasi hiki chini ya paa moja haikuwa rahisi,” Brandolino amewaambia washiriki. “Lakini hilo ndilo tulilohitaji hasa,” amesema, akisisitiza kuwa changamoto ya ulaghai wa kisasa inahitaji ushirikiano wa serikali, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa.

Teknolojia yabadilisha sura ya ulaghai

Brandolino amesema kuwa hali ya ulaghai imebadilika sana katika miaka ya hivi karibuni.

Uhalifu ambao hapo awali ulikuwa mdogo na wa ndani sasa umegeuka kuwa mitandao ya kisasa ya uhalifu inayofanya kazi katika nchi nyingi kwa wakati mmoja.

“Leo tunakabiliwa na aina tofauti kabisa ya ulaghai uliosheheni mbinu za kisasa, uliopangwa na unaotekelezwa kuvuka mipaka kwa kasi ya kushangaza,” amesema. “Walaghai wanaweza kuruka kutoka mamlaka moja hadi nyingine kwa sekunde chache, haraka zaidi kuliko vyombo vya sheria vinavyoweza kuchukua hatua.”

Ameongeza kuwa zana za kidijitali, sarafu za kidijitali kama vile cryptocurrency na majukwaa ya mtandaoni sasa yanawaruhusu wahalifu kuanzisha miradi ya ulaghai inayoweza kuwafikia mamilioni ya watu duniani kwa muda mfupi sana.

Mabilioni ya dola hupotea na waathiriwa kudhulumiwa

Kwa mujibu wa Brandolino, faida haramu zinazopatikana kupitia ulaghai ni kubwa sana, huku mabilioni ya dola yakiibwa kila mwaka kutoka kwa watu binafsi, biashara, taasisi na serikali.

“Pale panapokuwa na fedha za kupata, wahalifu watakuwa wa kwanza kuchangamkia fursa hiyo,” amesema, akiongeza kuwa tatizo hilo linazidi kuwa kubwa kutokana na mitandao ya uhalifu inayojipanga kwa ustadi zaidi.

Miongoni mwa mifano ya kutisha zaidi, amesema, ni uwepo wa viwanda vya utapeli vinavyotegemea wafanyakazi wanaosafirishwa kinyume cha sheria au kiharamu na kulazimishwa kufanya kazi.

“Baadhi ya mifano ya kutisha zaidi ni ile inayoitwa viwanda vya uaghai vinayotumia wafanyakazi waliotumikishwa kwa njia ya usafirishaji haramu wa binadamu,” amesema, akionya kuwa mfumo huo wa ulaghai unaanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali duniani.

Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu kukabiliana naulaghai

Brandolino amesisitiza umuhimu wa mifumo ya kisheria ya kimataifa inayoweza kusaidia nchi kushirikiana katika kukabiliana na ulaghai.

Mifumo hiyo ni pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifu wa Kimataifa wa Kupangwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa Ddhidi ya Uhalifu wa Mtandaoni ambayo ilianza rasmi kutiwa saini mwaka jana na tayari imesainiwa na nchi 74.

Amesema mikataba hiyo inaweka msingi muhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika uchunguzi na mashtaka ya uhalifu wa kuvuka mipaka.

“Kuna hatua tunazoweza kuchukua ambazo zinaweza kuleta mabadiliko kuna matumaini katika kupambana na aina hii ya uhalifu,” Brandolino amewaambia wajumbe wa mkutano huo.

Hatua za kimataifa dhidi ya ulaghai wa kupangwa

Katika siku mbili za mkutano huo, washiriki wanatarajiwa kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, kampuni za teknolojia, taasisi za fedha na mashirika ya kiraia ili kuzuia na kukabiliana vyema na ulaghai wa kifedha.

Majadiliano hayo yataangazia pia namna ya kuimarisha ushirikiano kati za sekta ya umma na binafsi, kulinganisha sera na mbinu za kiteknolojia pamoja na vyombo vya sheria, na kusaidia waathiriwa wa udanganyifu kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Brandolino amesema “Mkutano huu ni mwanzo tu. Ni fursa muhimu ya kuamua mwelekeo wa baadaye wa mapambano ya kimataifa dhidi ya ulaghai na kulinganisha juhudi zetu kuvuka mipaka, sekta na taasisi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *