
Utambulisho wa siasa za Tanzania baada ya chaguzi ni minyukano ya hoja, mijadala ya wananchi mitaani na katika mitandao ya kijamii na mikutano au matamko ya vyama vya siasa hasa hasa vya upinzani dhidi ya Serikali na chama tawala.
Lakini hali imekuwa tofauti, katika miezi ya karibuni kumeshuhudiwa utulivu usio wa kawaida katika uwanja wa siasa.
Mikutano mikubwa ya hadhara imepungua, mijadala ya kisiasa kwenye majukwaa ya umma imepotea, matamko ya vyama vya siasa imepotea na hata pale chama tawala kinapofanya shughuli za kisiasa kama ziara za viongozi wake hazigeuki mjadala mitandaoni kama ilivyokuwa.
Hata katika mitandao ya kijamii ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa uwanja wa mapambano ya kisiasa, mijadala wa hoja za vyama umeonekana kupungua.
Hiyo inaibua swali kuwa ukimya huo ni dalili ya utulivu au ishara ya changamoto katika demokrasia.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na utawala, wanataja sababu kadhaa za hali hiyo ikiwemo mabadiliko ya kimkakati ya vyama vya siasa, mazingira ya kisiasa na hadi uchovu wa mambo ya siasa miongoni mwa wananchi.
Mabadiliko ya mikakati ya vyama
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Baraka Mtemvu anaamini ukimya huo ni matokeo ya mabadiliko ya mikakati ya vyama vya siasa.
Kwa mtazamo wake, vyama vingi vinaonekana kupunguza shughuli za wazi wakati huu, badala yake vinawekeza katika maandalizi ya ndani.
“Katika kipindi hiki ambacho hakiko karibu sana na uchaguzi, baadhi ya vyama vinaamua kujipanga kimkakati zaidi kuliko kufanya siasa za majukwaani.
“Wanajenga mitandao yao ya ndani, wanafanya tathmini ya nguvu zao na kupanga mikakati ya muda mrefu,” anasema Dk Mtemvu.
Hali hiyo, anasema huenda ikaonekana kama ukimya kwa umma, lakini ndani ya vyama kunaweza kuwa na shughuli nyingi za kisiasa zisizoonekana hadharani.
Hata hivyo, anakiri kuwa tofauti na miaka ya nyuma, kiwango cha mijadala ya wazi ya kisiasa kimepungua.
Athari za mazingira ya kisiasa
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa na utawala, Said Majjid, anasema mazingira ya kisiasa yanaweza pia kuwa sababu inayochangia hali hiyo.
Katika mifumo mingi ya kisiasa duniani, anasema kiwango cha shughuli za kisiasa mara nyingi hutegemea jinsi vyama na wanasiasa wanavyotathmini mazingira ya kisiasa.
“Kama wanasiasa wanahisi mazingira si rafiki sana kwa mikutano mikubwa au mijadala mikali ya kisiasa, mara nyingi huamua kupunguza shughuli za aina hiyo,” anasema.
Anaeleza mazingira ya kisiasa yanaweza kujengwa na mambo mengi, ikiwemo sheria, kanuni, au hali ya kisiasa inayotawala kwa wakati husika.
Kwa mtazamo wake, iwapo vyama vinahisi mazingira ya kisiasa yanahitaji tahadhari zaidi, vinaweza kuchagua kuwa na sauti ya chini.
Anatolea mfano baadhi ya vyama nchini kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vinashindwa kufanya shughuli zao za kisiasa kwa sababu vinazuiwa kwa mujibu wa sheria.
“Unakumbuka kilijaribu kwenda kufanya kongamano la wanawake, walikamatwa. Sasa chama kama hiki sio kwamba kipo kimya, kimebadili mbinu za kufanya siasa kutokana na mazingira,” anasema mchambuzi huyo.
Wananchi wamechoka siasa
Sababu nyingine inayotajwa na wachambuzi ni kile kinachoitwa uchovu wa kisiasa miongoni mwa wananchi.
Mtaalamu wa sayansi ya siasa katika mtumishi katika moja ya taasisi za kimataifa, Dk Musa Kidevu anasema baada ya vipindi virefu vya mijadala mikali ya kisiasa katika miaka iliyopita, baadhi ya wananchi wanaweza kuwa wamechoshwa na kelele za siasa.
“Wananchi wanapokuwa wamepitia vipindi virefu vya migogoro au mijadala mikali ya kisiasa, mara nyingine huanza kutafuta utulivu zaidi kuliko mijadala mikali,” anasema.
Katika hoja yake hiyo, anasema hali hiyo inaweza kufanya hata wanasiasa kupunguza shughuli za kisiasa kwa sababu wanahisi wananchi hawana hamasa kwa wakati husika.
Anasema mabadiliko ya vipaumbele vya wananchi kama masuala ya uchumi, ajira na maisha ya kila siku, yanaweza kupunguza ushiriki wao katika mijadala ya kisiasa.
Kupungua kwa hoja
Moja ya mambo ambayo wachambuzi wanasema yanaonekana wazi ni kupungua kwa mijadala ya hoja kwa hoja kati ya vyama vya siasa.
Kwa miaka mingi, Dk Kidevu anasema siasa za Tanzania zilikuwa na mzunguko unaojirudia, chama kimoja kinatoa hoja, kingine kinajibu na mjadala unaendelea katika vyombo vya habari na majukwaa ya umma, lakini hilo halipo kwa sasa.
Kupungua kwa mijadala ya aina hiyo, anasema kunaweza kuathiri demokrasia.
“Demokrasia haiishi kwenye sanduku la kura pekee. Inaishi pia katika mijadala ya wazi ya sera na mawazo,” anasema.
Anaeleza mijadala ya kisiasa inapopungua, wananchi wanaweza kukosa fursa ya kusikia mitazamo tofauti kuhusu masuala ya kitaifa.
Anasema mijadala ya hoja kwa hoja pia husaidia kuboresha sera za umma kwa sababu mawazo mbalimbali yanapimwa na kuchambuliwa hadharani.
Athari kwa ushiriki wa wananchi
Mchambuzi wa siasa na historia, Juma Mwang’onde, anasema mijadala ya kisiasa mara nyingi ndiyo huchochea wananchi kufuatilia na kushiriki katika masuala ya utawala.
“Wananchi wanapokuwa hawasikii mijadala ya kisiasa mara kwa mara, kuna hatari ya kupungua kwa hamasa yao ya kufuatilia siasa,” anasema.
Anasema mjadala huo unasaidia wananchi kuelewa sera, kutathmini viongozi wao na kufanya uamuzi sahihi wanapopiga kura.
Mitandao ya kijamii
Katika miaka ya karibuni, mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa muhimu la mjadala wa kisiasa nchini, lakini hata huko, wachambuzi wanasema imepungua kwa kiwango kikubwa.
Dk Mtemvu anaeleza mabadiliko ya namna mitandao ya kijamii inavyotumika yanaweza kuwa sehemu ya sababu.
“Kwa sasa mijadala mingi katika mitandao ya kijamii imehamia zaidi kwenye masuala ya kijamii na kiuchumi kuliko siasa za vyama,” anasema.
Anaongeza kuwa baadhi ya wanasiasa, pia, wamekuwa waangalifu zaidi katika matumizi ya mitandao ya kijamii kutokana na athari zake katika taswira ya kisiasa.
Ukimya una madhara
Dk Mtemvu anasema demokrasia inahitaji ushindani wa mawazo na mijadala ya wazi.
“Kama hakuna mjadala wa kisiasa, kuna hatari ya kupungua kwa uwajibikaji wa viongozi,” anasema.
Anasema mijadala ya kisiasa mara nyingi ndiyo hutoa shinikizo la kijamii linalowalazimu viongozi kueleza sera zao na kuwajibika kwa wananchi.
Anaonya ukimya wa kisiasa unaweza kupunguza ubunifu wa sera mpya kwa sababu mawazo mapya mara nyingi hutokana na mijadala ya kisiasa.
Nini kifanyike?
Dk Mtemvu anasema vyama vinaweza kutumia majukwaa ya mijadala ya sera, makongamano na midahalo ili kuwashirikisha wananchi.
“Wananchi wanahitaji kusikia mawazo tofauti kuhusu uchumi, elimu, afya na masuala mengine ya maendeleo na hayo mara nyingi yanasikika kwenye majukwaa ya kisiasa,” anasema.
Katika hatua ya sasa, anasema ni muhimu kutafuta njia za kuhakikisha mijadala ya kisiasa inaendelea kwa njia nzuri, yenye heshima na inayosaidia maendeleo ya Taifa.
Kwa sababu katika mwisho wa yote, anaeleza nguvu ya demokrasia haipimwi kwa kuwepo kwa uchaguzi, bali kwa uhai wa mijadala ya kisiasa inayowawezesha wananchi kuelewa, kuuliza maswali na kushiriki kikamilifu katika mustakabali wa nchi yao.
Wasemavyo wanasiasa
Alipoulizwa kuhusu hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu anasema uchaguzi umevigharimu vyama fedha nyingi, zikiwemo akiba zao.
Kutokana na gharama hizo, anasema kwa sasa vyama vinajivuta na kujichanga ili vipate fedha za kufanya shughuli za kisiasa.
“Vyama vyetu havina ruzuku, hivyo baada ya uchaguzi tunajiunga upya, kwa sasa tunatafakari na kuangalia namna gani tunajipanga,” anasema Khatibu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ada-Tadea.
Khatibu aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama chake, anasemsa CCM inafanya shughuli kwa sababu ina vyanzo vya mapato na fedha.
“Tunatamani tufanye kazi ya siasa, lakini hali ya ukata ni kubwa kwa vyama vyetu,” anasema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita anakiri kupoa kwa siasa baada ya uchaguzi huku akitaja matukio ya Oktoba 29, 2025 kuwa sababu za hali hiyo.
Anaeleza matukio hayo, yalisababisha mijadala ya kisiasa igeuke kutoka kwenye masuala ya kawaida hadi kubadili mkondo uliosababisha watu wajadili hadi mapinduzi.
“Kuna wakati kulikuwa na matumaini kwamba kunaweza kutokea mapinduzi, pengine jeshi linaweza kuchukua nchi, kilikuwa kipindi kila mmoja alishangazwa na kilichotokea kwenye uchaguzi,” anasema.
Anasema ilionekana kuwa mkono wa kawaida wa siasa hauwezi kutawala kwa namna ya kukidhi matarajio ya wananchi, hiyo ilivifanya vyama vya siasa vitulie kwa ajili ya kuona namna gani vitatoa uongozi wa kuvuka.
Katika nyakati hizo, pia, anasema kulikuwa na matumizi ya nguvu ya dola iliyovifanya vyama vya siasa vizuri nyuma katika utekelezaji wa harakati zake, isingekuwa rahisi kuifanya siasa katika mazingira hayo.
“Pia, ni kipindi cha tafakuri kwamba nini tunaweza kufanya ili kwenda sawa. Angalau mwamko umeanza kurudi na kwa kadiri tunavyoenda huenda hali ikatengemaa,” anasema.