Taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa akiwa Brussels nchini Ubelgiji imemnukuu Guterres akieleza kuwa “Nimehuzunika sana kusikia taarifa za kifo cha Nicholas Haysom mwanasheria mwenye misimamo thabiti, mpatanishi asiyechoka, na mtetezi wa kudumu wa maadili ya Umoja wa Mataifa.”

Ameongeza kuwa “natoa pole zangu za dhati kwa familia yake na wapendwa wake, pamoja na wafanyakazi wenzetu wote waliobahatika kuvutiwa na mchango wake katika harakati za kuleta amani.”

Utendaji kazi wake

Akizungumzia kuhusu utendaji kazi yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Haysom alijitolea maisha yake katika kuhakikisha kuna haki, mazungumzo, na maridhiano kuanzia mchango wake muhimu katika mchakato wa mpito wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini, alipohudumu kama Mshauri Mkuu wa Sheria na Katiba wa Rais Nelson Mandela, hadi miaka mingi ya uongozi wake katika nyadhifa mbalimbali za Umoja wa Mataifa katika maeneo yenye changamoto na migogoro mikubwa duniani. 

Hivi karibuni zaidi, alihudumu kama Mkuu wa Ujumbe wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini. 

“Katika kila jukumu, aliunganisha umahiri wa kina wa kisheria na busara ya kisiasa, pamoja na kujitolea bila kuyumba katika kuboresha maisha ya watu.”

UN itakukumbuka

Guterres amesema “urithi wa Nicholas Haysom utaendelea kuishi kupitia michakato ya amani aliyosukuma mbele, taasisi alizoziimarisha, na misingi ya maadili aliyosaidia kuyaweka hai kote duniani.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *