Ripoti iliyotolewa Jumanne ya tarehe 17 Machi mwaka huu 2026 inasema vifo hivyo vingine ni kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika, na hii imesababisha maendeleo ya kimataifa kuhusu maisha ya watoto kupungua. Mashirika hayo yamesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu mwaka 2000, ambapo vifo vya watoto vilipungua kwa zaidi ya nusu, maendeleo hayo sasa yamepungua kwa kasi kubwa tangu mwaka 2015, hali inayotishia mafanikio patikana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo yenye jina ‘Levels & Trends in Child Mortality’, vifo vingi vya watoto vinatokana na sababu zinazoweza kuzuilika kwa gharama nafuu iwapo huduma bora za afya zitapatikana kwa wakati. Ripoti hiyo pia imeonesha kwa mara ya kwanza tathmini ya kina ya sababu kuu za vifo, ikiwemo mchango wa utapiamlo mkali, ambao umehusishwa moja kwa moja na vifo vya zaidi ya watoto 100,000 mwaka 2024.

Mashirika hayo yameonya kuwa athari halisi za utapiamlo ni kubwa zaidi kuliko takwimu zinavyoonesha, kwani hali hiyo hudhoofisha kinga ya mwili na kuongeza hatari ya watoto kufariki kutokana na magonjwa ya kawaida kama nimonia, kuhara na malaria. Nchi kama Pakistan, Somalia na Sudan zimeainishwa kuwa miongoni mwa zilizoathirika zaidi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa watoto wachanga wanabeba mzigo mkubwa zaidi wa vifo, wakichangia karibu nusu ya vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano. Sababu kuu ni pamoja na kuzaliwa kabla ya wakati, matatizo wakati wa kujifungua pamoja na maambukizi ya mapema. Baada ya kipindi cha mwezi mmoja wa kwanza, magonjwa ya kuambukiza yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo, hususan katika maeneo yenye rasilimali chache.

Kwa upande wa kijiografia, ripoti imebaini kuwa vifo vya watoto vimejikita zaidi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia ya Kusini, hali inayodhihirisha pengo kubwa la upatikanaji wa huduma za afya ikilinganishwa na maeneo kama Ulaya, Amerika Kaskazini na Oceania. Aidha, watoto wanaozaliwa katika nchi zilizoathiriwa na migogoro au hali tete wana uwezekano wa kufariki mara tatu zaidi kabla ya kufikisha miaka mitano.

Vijana

Mashirika ya Umoja wa Mataifa pia yameeleza wasiwasi kuhusu vifo vya vijana, yakibainisha kuwa zaidi ya watu milioni 2.1 wenye umri wa miaka 5 hadi 24 walifariki mwaka 2024. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sababu za vifo hutofautiana kulingana na umri na jinsia, ambapo kujidhuru ni chanzo kikuu kwa wasichana balehe na ajali za barabarani kwa wavulana.

Wakati huo huo, mashirika hayo yameonya kuwa kupungua kwa ufadhili wa maendeleo ya kimataifa kunaathiri juhudi za kuboresha afya ya mama na mtoto, na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya ya msingi pamoja na ukusanyaji wa takwimu ili kusaidia kupanga na kutekeleza afua stahiki.

Yakitoa wito wa hatua za haraka, mashirika hayo yamesisitiza kuwa uwekezaji katika afya ya watoto ni mojawapo ya hatua zenye manufaa makubwa kiuchumi na kijamii, ambapo hata afua rahisi kama chanjo, lishe bora na huduma salama za kujifungua zinaweza kuokoa mamilioni ya maisha.

Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell amesema hakuna mtoto anayepaswa kufa kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika, huku akionya kuwa kupungua kwa kasi ya maendeleo kunakuja wakati ambapo rasilimali zinapungua.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesisitiza kuwa licha ya maendeleo yaliyofikiwa, bado watoto wengi wanapoteza maisha kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika, hasa katika maeneo yenye migogoro na changamoto za kibinadamu.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, ripoti hii ni wito wa dharura kwa serikali, wafadhili na wadau wote kuongeza juhudi na uwekezaji, ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kuishi na kustawi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *