BUKOBA: Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Johnston Mutasingwa, ametoa msaada kwa makundi maalumu pamoja na wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Kata ya Kibeta katika kipindi mwezi wa Ramadhan na Kwaresma.
Mahitaji yaliyotolewa ni sukari, sabuni na vyakula mbalimbali vya kusaidia familia kipindi cha mfungo. Msaada huo ulikabidhiwa na katibu wake Hamada Simba.

Simba amesema msaada huo unalenga kuwasaidia wananchi walio katika mazingira magumu, wakiwemo wazee, watu wenye ulemavu pamoja na kaya zenye kipato cha chini zinazofaidika na mpango wa TASAF.

Wananchi walionufaika na msaada huo walionyesha furaha na shukrani zao za dhati kwa mbunge wao, wakisema kuwa hatua hiyo imewapa faraja kubwa na kuwasaidia kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.
“Tunamshukuru sana mheshimiwa mbunge kwa kutujali, msaada huu umekuja wakati sahihi na utatusaidia sana katika maisha yetu,” amesema mmoja wa wanufaika.

Diwani wa Kata kibeta, Anastella Alphuns amesema kuwa kwa ujumla, tukio hilo limeendelea kuonesha mshikamano kati ya viongozi na wananchi pamoja na juhudi zinazoendelea za kuhakikisha ustawi wa jamii unaimarika, hasa kwa makundi yenye uhitaji zaidi.
