
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika taasisi za gesi na nishati za Iran pamoja na shambulio katika kisima cha gesi cha Pars-Kusini na katika eneo la Asaluyeh.
Farhan Haq amesisitiza udharura wa Marekani na Israel kujiepusha kuwalenga raia nchini Iran na kusema: Tunataka kuwa na uhakika kwamba taasisi na miundo msingi ya kiraia haishambuliwi.
Kuhusu kuuawa shahidi viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwemo Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa taifa, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa pia amesema: Umoja wa Mataifa, ikiwa taasisi ya ngazi ya juu, unapinga hatua yoyote iliyosawa na kutekeleza mauaji nje ya mkondo wa sheria; na hili liko wazi katika masuala yote.
Farhan Haq aidha amebainisha kuwa: Tunaamini mgogoro huu hauwezi kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kijeshi, na kwa mara nyingine tena tunazitaka Israel na Marekani ziache kushadidisha mashambulizi haya.