
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa vita vya sasa si vita vya wananchi wa Marekani. Ismail Baqaei ameeleza haya katika ujumbe aliotuma katika mtandao wa kijamii wa X baada ya kujiuzulu Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi wa Marekani, Joseph Kent.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa kutangaza kuchukizwa na kupinga vita hivi vilivyo kinyume cha sheria ni kazi ambayo kwa uchache inaweza na inapasa kufanywa na kila raia au kiongozi wa Marekani mwenye dhamiri ya mwamko.
Joe Kent alituma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X na kutangaza kujizulu kwake akisema kwamba: ” Siwezi kuunga mkono vita vinavyoendelea nchini Iran. “Iran si tishio la moja kwa moja kwa Marekani na ni wazi kwamba tumeanzisha vita hivi kutokana na mashinikizo ya Israel, kwa hivyo ninajiuzulu wadhifa wangu.” Ameongeza kwa kusema: “Nimeamua kujiuzulu kwa sababu siwezi kuunga mkono vita vinavyoendelea dhidi ya Iran.”
Katika barua yake kali kwa Rais Donald Trump, Mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi cha Marekani amesema: Maafisa wakuu wa Israel na watu kadhaa wenye ushawishi katika vyombo vya habari vya Marekani walianzisha kampeni iliyopangwa ili kupotosha umma. Kampeni hiyo ilitumika kukudanganya uamini kwamba Iran ni tishio la moja kwa moja kwa Marekani.