Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi kutoka Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), David Sukali, amesema mfumo wa stakabadhi za ghala umeendelea kuwa mkombozi kwa wakulima nchini kwa kuwapatia uhakika wa soko, bei na ubora wa mazao yao.

Akizungumza kuhusu mfumo huo, Sukali ameeleza kuwa stakabadhi za ghala ni mfumo wa kisheria ulioanzishwa mwaka 2005, huku kanuni zake zikikamilika mwaka 2006 na kuanza kutumika rasmi. Alibainisha kuwa kabla ya hapo kulikuwepo mifumo mbalimbali ya mauzo ya mazao tangu kipindi cha uhuru, lakini ilikumbwa na changamoto nyingi na mabadiliko ya mara kwa mara.

“Ilipofika mwaka 2000, Serikali iliona umuhimu wa kuwa na mfumo rasmi utakaowawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa utaratibu unaoeleweka na unaowalinda,” amesema Sukali.

Akizungumza jijini hapa, amefafanua kuwa stakabadhi ni nyaraka rasmi yenye taarifa muhimu za muweka mali ambaye amepeleka mazao yake katika ghala linalotambuliwa na kusimamiwa na bodi hiyo. Kupitia mfumo huo, wakulima hupata uhakika wa usalama wa mazao yao pamoja na soko lenye ushindani.

Sukali alisema kuwa ingawa kuna maghala mengi nchini, ni yale tu yanayokidhi vigezo maalum vya kisheria ndiyo huruhusiwa kutumika katika mfumo huo. Ameeleza kuwa ghala hilo lazima lipitie ukaguzi wa bodi na kupewa leseni rasmi ili liweze kufanya kazi chini ya mfumo wa stakabadhi za ghala.

“Tunayo fomu maalum namba mbili yenye masharti yote muhimu. Ili ghala lipewe leseni, lazima liwe na bima dhidi ya moto na wizi, pamoja na dhamana ya utendaji kuhakikisha usalama wa mali za wakulima,” amesisitiza.

Aidha, ameeleza kuwa ghala linalotaka kushiriki mfumo huo linapaswa kuwa na wafanyakazi wasiopungua watano waliopatiwa mafunzo maalumu. Wafanyakazi hao ni pamoja na mtunza stoo, mtaalamu wa mizani anayehakikisha uzito sahihi wa mazao, pamoja na mtaalamu wa kumbukumbu anayehifadhi taarifa muhimu kama ubora, aina ya zao na jina la mmiliki.

Katika utekelezaji wake, Sukali amesema mfumo huo unahusisha pia maghala ya awali yanayotumiwa na vyama vya ushirika kukusanyia mazao kutoka kwa wakulima kabla ya kuyapeleka katika ghala kuu lililopewa leseni na bodi.

Ameongeza kuwa baadhi ya mazao pia yanasimamiwa kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama COPPRA ili kuhakikisha usimamizi unakuwa madhubuti zaidi katika mnyororo mzima wa thamani.

Kwa upande wa soko, Sukali mesisisitiza kuwa mfumo huo unawaunganisha moja kwa moja wakulima na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi, hali inayochochea ushindani na kuongeza thamani ya mazao.

“Wanunuzi wanapata bidhaa zenye ubora unaokubalika kwa sababu kuna mamlaka zinazosimamia viwango. Hii inawasaidia wakulima kupata bei nzuri na kuongeza tija katika uzalishaji,” amesema.

Amebainisha kuwa WRRB imekuwa chombo muhimu cha Serikali katika kupunguza migogoro kati ya wakulima na wanunuzi, kwa kuweka mifumo ya uwazi na haki katika biashara ya mazao.

Sukali amehitimisha kwa kusema kuwa kwa kila msimu wa mauzo, bodi hiyo huandaa miongozo maalumu ya kusimamia na kuendesha zoezi la mauzo ili kuhakikisha mfumo unaendelea kuwa na tija na manufaa kwa wadau wote.

Akizungumzia mafanikio ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa WRRB, Dominic Dionis amesema ni pamoja na kusimamia upimaji sahihi wa mazao, ikiwamo ubora wake, tofauti na zamani walipokuwa wakipima kwa kutumia ndoo.

Amesema mafanikio mengine ni wakulima kuwa na uhakika wa soko na mahali pa kuhifadhi mazao yao.

“Zamani, kabla ya uwepo wa WRRB, wakulima walikuwa wanauza mazao shambani. Baadhi yao walikuwa wanauza shamba zima kwa bei ya hasara kwa sababu hata wakisubiri kuvuna walikuwa hawana pa kuhifadhi. Lakini sasa wanajua watahifadhi wapi na watauza muda wanaotaka wao kulingana na kupanda na kushuka kwa bei mnadani,” amesema Dionis.

Amefafanua kuwa mfumo huo pia unahusisha utoaji wa leseni au usajili wa mameneja dhamana ambao huwawezesha wakulima kupata fedha hata kabla ya kuuza mazao yao.

“Hawa mameneja dhamana jukumu lao ni kumkutanisha mkulima na taasisi za kifedha, ambapo hukopeshwa fedha hata kama hajauza mazao yake, kwa dhamana ya mazao yaliyohifadhiwa ghalani. Anaweza kukopeshwa fedha kwa bei ya mnada iliyopo wakati huo. Kisha yeye, meneja dhamana na wakopeshaji hufuatilia mwenendo wa bei mnadani. Ikitokea bei inapanda zaidi ya aliyokopeshwa, huwasiliana na kuuza, wakitoa gharama husika na kilichobaki mkulima huongezewa,” amesema Dionis.

Amesema mafanikio mengine ni kufungua fursa za ajira kwa vijana, ambapo katika kila ghala kuna watumishi wasiopungua watano, wabebaji zaidi ya 50 na watoa huduma mbalimbali, hivyo kufanya kila ghala kuwa na vijana wasiopungua 100.

Pamoja na mafanikio hayo, Dionis amesema wanatarajia kuongeza bidhaa nyingine tofauti na mazao, ikiwamo asali na mifugo hai.

“Kwenye mifugo hai tutashirikiana na ranchi za wanyama, ambapo mmiliki anapopeleka mifugo kuhifadhiwa ranchi itatambuliwa na kuwekwa mnadani ili wateja waweze kuiona,” amesema Dionis.

Amesema maadhimidho ya miaka 20 ya mfumo huo yatafanyika jijini Dodoma kuanzia Aprili 28 hadi 30 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *