Wakizungumza wakati wa kikao cha kando kwenye Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70 jijini New York, Marekani, chama hicho kimesema kinafanya hivyo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono mageuzi ya mahakama nchini Tanzania.

Kikao hicho cha kando kilikuwa na maudhui Kutatua vikwazo vya kijinsia kwenye haki kupitia mahakama ya mtandao nchini Tanzania, ambapo wametaja mageuzi hayo kuwa ni pamoja na mifumo ya kidijitali na mahakama za mtandaoni.

Muda wa kusikiliza kesi umepungua

“Kupitia uwekezaji katika teknolojia na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA, mahakama nchini Tanzania zinaendelea kuwa jumuishi zaidi, zenye ufanisi, na rafiki kwa watumiaji—hasa wanawake na manusura wa ukatili wa kijinsia, (GBV),” amesema Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Barke Sehel ambaye pia ni Mwenyekiti wa TAWJA iliyoanzishwa mwaka 2000 na kusajiliwa rasmi mwaka 2022

“Hatua kubwa iliyopigwa ni pamoja na uhifadhi wa kidijitali wa zaidi ya mafaili 10,000 ya zamani jijini Dar es Salaam, jambo lililopunguza muda wa kutafuta mafaili kutoka wiki kadhaa hadi dakika chache. Maboresho haya yameongeza kasi ya upatikanaji wa haki na kupunguza ucheleweshaji wa kesi unaowaathiri zaidi wanawake na makundi yaliyo hatarini,” amesema Mwenyekiti huyo wa TAWJA.

Kiini cha mabadiliko ni nini?

Kiini cha mabadiliko haya ni Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (JoT e-CMS), unaorahisisha shughuli zote za mahakama kwa njia ya kidijitali.

“Mfumo huu unaruhusu ufungaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (e-filing), ufuatiliaji wa kesi kwa wakati halisi, na upatikanaji wa kumbukumbu za kesi kwa urahisi.” Amesema Jaji Sehel.

Halikadhalika mfumo huo umewezesha kupanga kazi kiotomatiki ikiwa ni pamoja kugawa kesi kwa majaju, kupanga ratiba za usikilizwaji, na utoaji wa taarifa kwa wahusika. “Faida zake ni pamoja na upatikanaji wa huduma saa 24, kupunguza gharama za uendeshaji, na kupunguza makosa ya kibinadamu katika usimamizi wa kesi,” amefafanua Mwenyekiti huyo wa TAWJA.

Faida za mahakama mtandao

Wanawake wa Tanzania waliohudhuria mkutano wa CSW70, wakiwa wameketi kwenye jopo lenye maikrofoni na kompyuta ndogo, wakijadili haki na haki.

Ujumbe wa Tanzania kwenye kikao cha kando cha CSW70 jijini New York, Marekani, kuhusu Kutatua Vikwazo vya Kijinsia kwenye haki kupitia Mahakama Mtandao.

Wakati wa kikao hicho iliwekwa bayana ni kwa kiasi gani TEHAMA inaboresha haki pamoja na matumizi ya akili mnemba au AI katika kurekodi, kutafsiri, na kushughulikia ushahidi.

“Hii imepunguza kwa kiasi kikubwa maumivu ya kisaikolojia kwa manusura wa GBV kwa kuepusha kurudia simulizi za matukio yanayowapatia kiwewe,” amesema Jaji Sehel.

Faida zingine za mahakama mtandao ni kesi kuruhusu mashahidi kushiriki kesi wakiwa mbali, ndani na nje ya nchi. Aidha, katika makao makuu ya Mahakama yaliyopo Dodoma,mji mkuu wa Tanzania, yana  chumba maalum cha Kanzi Data au Data Hub kinachowezesha uchambuzi wa taarifa za kesi kwa wakati halisi, ikiwemo kesi za GBV.

Jambo lingine ni mfumo wa “Sema na Mahakama” unaotoa fursa kwa wananchi kutoa maoni au malalamiko kupitia simu au mtandao, huku Programu ya Mahakama za Mwanzo ikitoa takwimu za moja kwa moja kwa ajili ya ufuatiliaji na maamuzi.

Kuwezesha Wanawake Kupitia Haki za Kidijitali

Tanzania Women Judges Association imesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia si tu kuboresha utendaji bali pia ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha haki za wanawake zinazingatiwa. Kupitia mifumo hii, gharama zinapungua, faragha inaongezeka, na mazingira ya haki yanakuwa salama zaidi kwa wanawake.

Hata hivyo, chama hicho kimeonya kuwa matumizi ya teknolojia yanapaswa kuzingatia usawa ili kuepuka kuongeza changamoto mpya kwa makundi yaliyo pembezoni.

Teknolojia isijenge ukuta kati ya wa mijini na vijijini

Ni kwa mantiki hiyo Sara Omar Hafidh, Hakimu wa Mkoa, Zanzibar na pia Mratibu wa TAWJA huko Zanzibar amezungumzia umuhimu wa mafunzo endelevu kwa watendaji wa Mahakama.

“Sote tunajua kuwa kujifunza kubonyeza kitufe sahihi kwenye kompyuta ni jambo rahisi. Lakini sehemu ngumu ni kuendesha mahakama ya mtandaoni kwa huruma na uelewa. Tunawafundisha majaji na mahakimu wetu kushughulikia majeraha ya kisaikolojia kupitia skrini, kuhakikisha kwamba hata katika mazingira ya kidijitali kila mwananchi anahisi kuonekana, kusikilizwa, na kuheshimiwa,” amesema Mratibu huyo wa TAWJA, Zanzibar.

Jambo lingine ni kuhakikisha mifumo ya kidijitali ina ulinzi madhubuti wa taarifa.” Ni dhahiri kuwa mtu aliye katika hali ya hatari akihisi kuwa taarifa zake binafsi zinaweza kuvuja, ataogopa kujitokeza. Hivyo, dunia yetu ya kidijitali lazima iwe salama na isiyopenyeka. Teknolojia inapaswa kuwa ngao ya ulinzi—ngao inayowalinda walio dhaifu, si mwanga unaowaweka wazi,” amesema.

Mafunzo yanayotolewa na TAWJA

Kwa Dkt. Patricia Kisinda, Mkurugenzi wa Mafunzo, IJA na ni Katibu Msaidizi wa TAWJA amesema chama hicho ndicho cha kwanza kuanzisha mafunzo kwa watendaji wa Mahakama nchini Tanzania miaka ya 2000.

“Mafunzo haya yanayotolewa kwa ushirikiano na Mahakama ya Tanzania yanalenga pamoja na mambo mengine kujenga uwezowa majaji, mahakimu, waendesha mashtaka,askari polisi, magereza na wachunguzi wa kesi,” amesema.

Kupitia mafunzo hayo, washiriki hupewa maarifa na ujuzi wa vitendo unaohitajika kushughulikia kesi zenye mwelekeo wa kijinsia, ikiwemo ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa kingono, talaka na migogoro ya ndoa, ukatili dhidi ya watoto na matunzo yao, pamoja na masuala ya mirathi, na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Washiriki pia hufundishwa jinsi ya kuepuka kuongeza maumivu ya kisaikolojia kwa manusura wa unyanyasaji wa kingono na ukatili wa kijinsia, kwa kudhibiti mwenendo wa mahakama na kukusanya ushahidi kutoka kwa manusura kwa njia inayolinda utu wao, ili kufikia maamuzi ya haki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *