Maelfu ya wakimbiaji kutoka ndani na nje ya Tanzania, wanaendelea kumiminika katika mji wa Moshi kushiriki Kilimanjaro International Marathon inayotarajiwa kufanyika Jumapili hii ya Machi 22, 2026. Tukio hili ambalo hufanyika kila mwaka limeendelea kuifanya Tanzania kuwa kituo cha michezo na utalii duniani.

Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania ambayo inadhamini kilomita 21 yaani ‘Yas Kili International Marathon’ kwenye mashindano hayo makubwa, imesema imejipanga kikamilifu kuhakikisha hakutokei tatizo lolote la kimtandao.

Kila mwaka, mbio hizo hukutanisha wanariadha wengi, wakiwemo wenye ujuzi wa juu na wakimbiaji wa kawaida, hivyo kuongeza hadhi ya Tanzania katika ramani ya michezo ya kimataifa.

Mbio hizo zina marathon kamili ya km 42.2, nusu marathon km 21.1 na mbio za km 5 zinazojulikana kama Fun Run.

Mashindano haya yanachangia moja kwa moja maendeleo ya jamii. Faida za udhamini, michango na ada za ushiriki husaidia kuboresha elimu, huduma za afya na kuendeleza vipaji vya vijana katika michezo.

Ushirikiano huu unachochea mshikamano wa kijamii na maendeleo endelevu katika jamii za mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla.

Pia ni kichocheo kikubwa cha utalii na uchumi. Wageni kutoka nje hutumia fursa ya kushiriki au kutazama, kisha kutembelea vivutio vingine kama Serengeti na Ngorongoro.

Biashara za ndani, ikiwemo hoteli, migahawa, maduka na huduma za usafiri, hupata wateja wengi na hivyo kuongeza mapato na kukuza uchumi wa mji wa Moshi na maeneo ya jirani.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Yas Tanzania, Amos Bwire, ameeleza kuwa mtandao wa mawasiliano ni muhimu sana kwa mashindano haya. Upatikanaji wa mtandao wa uhakika unawawezesha washiriki na watazamaji kushirikisha matukio, picha na video kwa wakati halisi.

Alifafanua kuwa si kwa upande wa burudani pekee, bali hata uendeshaji wa mashindano unategemea sana mtandao.

“Wakati wa mbio, mifumo ya kupima muda, kufuatilia utendaji wa wakimbiaji pamoja na matumizi ya programu za matukio yote yanahitaji upatikanaji wa mtandao wa uhakika,” alisema.

Bwire pia aligusia mchango wa wanahabari na waundaji wa maudhui, akisema: “Vyombo vya habari na ‘content creators’ wanahitaji mtandao wenye kasi ili waweze kusambaza taarifa, picha na video kwa wakati halisi.”

Aidha, alisisitiza kuwa mawasiliano bora yana nafasi muhimu katika usalama wa mashindano: “Waandaaji wanahitaji mawasiliano ya uhakika kuratibu huduma za usalama na timu za matibabu katika njia yote ya mbio. Hii inasaidia kuhakikisha usalama na hatua za haraka za dharura endapo zitahitajika.”

Akizungumzia maandalizi ya kiufundi, Bwire alisema mashindano makubwa kama hayo huongeza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mtandao.

“Tumefanya tathmini ya uwezo wa mtandao na utabiri wa matumizi kwa kuchambua takwimu za matukio yaliyopita ili kuelewa mahitaji ya mwaka huu, hivyo tumeboresha,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *