Dar es Salaam. Kuna wakati watoto wa mjini walipiga hela kiulaini sana. mtu aliivizia nguzo ya umeme usiku pasipo na watu, akaibandika karatasi lililoandikwa “Mpigie Mganga wa Ndoto”. 
Chini akaweka namba kwa maandishi makubwa na wino uliokolezwa zaidi. Watu wakaota, wakapiga simu naye akawajibu baada ya muamala wake kusoma. Ni rahisi sana, haina Brela wala TRA.

Kumbe hawa jamaa walitumia mbinu inayotumiwa na waganga wa vijijini. Wagonjwa wao wanaumwa matumbo kwa sababu ya maji machafu.

Wanawaambia wametupiwa majini, kisha wanawapa mzizi wowote na kuwaagiza wachemshie kwenye maji ili kumwondoa jini. Hivyo wanakijiji wanakunywa maji safi na salama, na hawataumwa tumbo tena.   

Vivyo hivyo katika ndoto, kila mtu ana zake. Lakini kwa sababu ndoto zote ni zilezile, inatafutwa sababu ya ndoto ya mtu mmoja mmoja na nyimbo zinaanzia hapo. 
Bodaboda anaota akirusha helikopta, chinga anaota akimiliki soko la Kariakoo, hata mraibu naye ana ndoto zake, kubwa ni ile ya kumiliki mjengo Oman. Kwa kifupi, ndoto zimekuwa matarajio ya kila mtu aliye hai hapa duniani.

Hebu tujiulize, ndoto ni nini hasa? Kwa lugha rahisi, ndoto (njozi) ni picha, mawazo au matukio yanayotokea akilini wakati wa usingizi. Ni kama sinema ya bure inayochezwa kichwani mwako bila bando. Leo unaweza kujikuta unakimbizwa na simba, kesho unakula pilau na rais, na kesho kutwa unaruka juu ya paa la nyumba kama kuku. 

Lakini kuna upande mwingine wa ndoto kuna ndoto za maisha (aspirations). Hizi si zile za usingizi, bali ni matarajio, malengo na tamaa za mtu. Ndoto ya kuwa daktari, kuwa tajiri, au hata kununua kiwanja Bunju. Hizi ndizo ndoto tunazopenda kujadili vichwani mwetu nyakati za mchana, tofauti na zile za usiku ambazo mara nyingi zinatufanya tuamke na jasho.

Wataalamu wanasema ndoto hutokana na mambo kadhaa, lakini tutaziweka kwa lugha ya mtaani. Jambo la kwanza ni kuwaza kitu kupita kiasi. Ukilala ukiwaza hela, uwezekano mkubwa utaota unahesabu noti au unaibiwa. Ukilala ukiwaza jambo fulani usilopenda likutokee, utaliota na si ajabu likakuhangaisha siku nzima. Kwa mawazo yako utadhani umeshushiwa maono au utabiri.

Kuna wahuni (samahani nisiwaite hivyo, pengine hata mimi nilikuwamo) walipiga swaga za “Usiku silali nakuota wewe tu…” Sasa wewe hulali, unawezaje kuota? Bila shaka tulichanganya ndoto na mawazo. Kila kimojawapo kati ya hivyo viwili kinaweza kusababishwa na kinginecho; ndoto inaweza kukuletea mawazo, na mawazo yanaweza kupelekea ndoto. Lakini ni vitu tofauti kabisa. 

Kitu cha pili kinachoweza kusababisha ndoto ni msongo wa mawazo (stress). Ukisongwa na maisha, akili hujaribu “kucheza sinema” ili kutoa presha. Ndiyo maana unaweza kuota unafukuzwa na watu au unaanguka bila mwisho. 

Waaguzi wa ndoto huwapenda sana watu wenye ndoto kama hizi, kwa sababu hawaumizi vichwa kupata hela zao. Sanasana watawashauri namna ya kuepukana na mawazo yao wenyewe. 

Kitu kingine ni vyakula na mazingira. Ukila hovyo usiku ni hatari kwa usingizi wako, lakini pia zingatia ndoto za anayelala kwenye tanda la sita kwa sita lenye godoro laini, haziwezi kufanana na anayelalia kitanda cha chuma. Tena kitanda chenyewe ni cha futi mbili kwa nne kisicho na godoro. Ndio pale unapoota uko uchi shuleni, huku mwalimu anakuita ubaoni akikunyoshea bakora ya tawi la mpera.

Lakini mara nyingi zaidi ndoto zinaletwa na kumbukumbu za siku. Mambo unayoyafanya mchana yanajirudia usiku, lakini yakijiongoza kivingine kabisa. Ukiondoa sababu ngumu kama msongo, mara nyingi tunaota mambo yaleyale na watu walewale. Tofauti unakuwa ni mpangilio tu. Ukiwa kibarua mchanganya zege, unaweza kujikuta ndiye bosi mwekezaji ukiwa ndotoni.  

Tatizo neno “ndoto” linachukuliwa kirahisi sana. Limekuwa kama salamu ya kawaida kwa mtu kusema “ndoto yangu ni utajiri”. Mtu huyo anaweza kuwa hana hata mpango wa kesho. Ni ndoto ya kusema tu, kama vile mtu anavyosema “nitakunywa chai kesho” halafu kesho yake anapiga ndefu bila kula chochote hadi mchana. Ndoto aliyosema haimshughulishi maana si deni, na anaweza akaitamka tena bila kushtakiwa.

Wapo pia wale wa ndoto zisizo na miguu wala kichwa kama Alinacha. Mtu hana mtaji, hana mpango, hana hata akaunti ya benki, lakini ndoto yake ni kuwa bilionea “kabla mwaka haujapinduka”. Watu wana masihara sana, eti walevi nao wanaalikana baa kwa kusema: “Njoo tutengeneze ndoto…” 

Hapo ndoto haimaanishi ile ya usingizi wala ya maisha, bali ni kuwaza kisichokuwepo (au kuondoa mawazo).

Zamani zile za “Maprofesa” wa kutafsiri wa ndoto, magazeti yote yalibeba kurasa zao wakichukua ndoto kwa uzito wa ajabu. Ukimwambia kuwa umeota kuku, anaweza kukuambia ujiandae kwa wageni au pesa. Ukimwambia umeota unakimbizwa, tayari anakuwekea tahadhari ya wachawi.

Kwa kifupi, ndoto zilikuwa na nguvu zaidi ya sasa. Leo mtu anaota anafukuzwa na mbwa, anaamka na kusema: “Ah, nilikula sana jana.”
Usipate taabu: Kula na kunywa kwa kiasi, lala unono kwa muda wa kutosha, fanya kazi uipendayo na uridhike nayo. Hakika utaota paradiso!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *