Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali inazidi kuwa mbaya kutokana na kuongezeka kwa machafuko kaskazini mwa Sudan Kusini, kupungua kwa misaada ya kibinadamu, pamoja na hali ngumu ya uchumi na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri uzalishaji wa chakula.
Katika hospitali ya serikali mjini Bor, mtoto wa miezi 14, Adut Duor, anaakisi uhalisia wa janga linaloshuhudiwa. Mtoto huyo anayeonekana dhaifu huku Uti wake wa mgongo ukiwa umechomoza nje ya ngozi na miguu yake imekondeana . Mama yake, Ayan, hawezi kumnyonyesha kutokana na utapiamlo uliomkumba, hali inayowakabili pia wanawake zaidi ya milioni 1.1 wajawazito na wanaonyonyesha nchini humo.
Mashirika ya misaada kama Save the Children yamelazimika kufunga baadhi ya vituo vya afya na kupunguza wafanyakazi wake kutokana na kukosekana kwa ufadhili. Katika hospitali ya Bor pekee, visa vya utapiamlo vimeongezeka zaidi ya mara mbili mwaka huu, huku chakula tiba (RUTF) kikielekea kuisha.
Clement Papy Nkubizi, Mkurugenzi wa shirika la Action Against Hunger nchini Sudan Kusini, anasema asilimia 22 ya watoto waliolazwa kwa utapiamlo katika hospitali ya Juba wamepoteza maisha. Na idadi inaweza kuwa juu zaidi endapo watahusisha maeneo ya vijijini. Christopher Nyamandi, ni Mkurugenzi wa Save the Children Sudan Kusinianasema hapajakuwa na mavuno mazuri kutokana na mafuriko katika baadhi ya maeneo.
“Familia hazina chakula. Hakujakuwa na mavuno mazuri katika miaka miwili iliyopita kutokana na mafuriko katika baadhi ya maeneo, lakini pia kutokana na uwekezaji mdogo katika kilimo na shughuli za kujikimu kote nchini. Zaidi ya watu milioni 9 wamekuwa wakitegemea msaada wa kibinadamu. Hivyo basi, kupunguzwa kwa misaada kumeathiri sana hali yetu kwa sababu hii ni nchi iliyokuwa ikitegemea zaidi msaada.”
Migogoro inatatiza shughuli za kupeleka misaada ya kiutu
Wakati misaada inapungua, machafuko mapya katika majimbo ya Upper Nile na Jonglei yamezuia usafirishaji wa chakula na dawa. Mamia ya maelfu ya watu wamelazimika kuyaacha mashamba yao, na zaidi ya watoto 60,000 wameachwa bila msaada kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Mafuriko pia yameharibu maghala ya misaada na kusababisha mashamba kufurika, hali inayowaweka watu milioni 1.6 kwenye hatari ya kuhama makazi. Maji machafu yamechochea kuenea kwa kipindupindu, malaria na kuhara, hali inayoongeza vifo vya watoto. Katika hospitali ya Maban kaskazini mwa Sudan kusini, Moussa Adil, mtoto wa miezi minane, analia kwa njaa huku mama yake akiwa hana msaada wowote. Hakuna maziwa ya lishe na wauguzi wengi hawajalipwa kwa zaidi ya miezi sita.
Wakati hayo yakiendelea, serikali ya Sudan Kusini imeendelea kupuuzwa kwa matumizi ya ndani kwenye afya na lishe. Ripoti ya UNICEF inaonesha kuwa serikali hutenga asilimia 1.3 pekee ya bajeti yake kwa sekta ya afya, mbali na lengo la asilimia 15 linaloainishwa na Shirika la Afya Duniani.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Yasmin Sooka ametaja kuwa mabilioni ya dola yameporwa na viongozi wa serikali kupitia Ufisadi. Kwa sasa, hali inaendelea kuwa mbaya. Watoto kama Adut na Moussa wanasubiri msaada ambao haujulikani utaifika lini — huku maisha yao yakiwa yananing’inia kwa uzi mwembamba kati ya maisha na mauti.
