
Katika taarifa yao kutoka New York Marekani, Kinshasa Congo na Kampala Uganda UNICEF imesema, “kila mlipuko wa Ebola huwaweka watoto hatarini si tu kutokana na ugonjwa wenyewe, bali pia kuvurugika kwa huduma muhimu kama afya, lishe, elimu na ulinzi.”
Shirika hilo linaeleza kuwa linashirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha juhudi za kudhibiti maambukizi zinafanyika haraka, huku likisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii na uratibu wa mipakani.
Hatua walizochukua
UNICEF tayari imechukua hatua kadhaa za haraka kukabiliana na mlipuko huo.
“Hatua za haraka, ushirikiano wa jamii, na kuimarisha nguvu ya wahudumu wa afya ni muhimu ili kulinda watoto na kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huu.” Imesema taarifa yao
Shirika hilo limepeleka takribani tani 50 za vifaa muhimu vya kudhibiti maambukizi, vikiwemo:
- Sabuni na dawa za kuua vijidudu,
- Vifaa kinga binafsi (PPE),
- Vidonge vya kusafisha maji na matangi ya kuhifadhi maji.
Pia, zaidi ya wahudumu wa afya wa jamii 2,000 wameshapangiwa kazi ya kuelimisha wananchi na kutoa huduma katika maeneo hatarishi, huku timu maalum ya dharura ikitarajiwa kuwasili kusaidia juhudi hizo.
Athari kwa watoto
UNICEF imeonya kuwa watoto wako katika hatari kubwa si tu ya kuambukizwa Ebola, bali pia athari za kijamii na kiakili. Wanakabiliwa na:
- Kupoteza wazazi au walezi,
- Kusitishwa kwa masomo,
- changamoto katika huduma za afya na lishe,
- pamoja na unyanyapaa na msongo wa mawazo.
Wito kwa jamii na dunia
UNICEF imetoa wito kwa:
- Kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa usalama katika maeneo yaliyoathirika,
- Kuimarisha elimu kwa jamii kuhusu njia za maambukizi na kinga,
- Kuongeza rasilimali kwa wahudumu wa mstari wa mbele.
Kadri mlipuko huu unavyoendelea, UNICEF inasisitiza kuwa ushirikiano wa haraka kati ya serikali, mashirika na jamii ni nguzo muhimu katika kudhibiti ugonjwa huu. Lengo kuu likibaki kuwa moja: kuwalinda watoto na kuokoa maisha.
