FAO yaadhimisha Siku ya Nyuki Duniani 2026 kwa wito wa kulinda wachavushaji na usalama wa chakula dunianiFAO yaadhimisha Siku ya Nyuki Duniani 2026 kwa wito wa kulinda wachavushaji na usalama wa chakula duniani

Katika maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani 2026 yanayofanyika leo tarehe 20 Mei, FAO imesema siku hiyo inalenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa nyuki pamoja na hatari zinazotishia maisha ya wachavushaji duniani.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Bee Together for People and the Planet – A Partnership That Sustains Us All” ambayo kwa Kiswahili inaweza kutafsiriwa kama “Tushirikiane kwa Ajili ya Watu na Sayari – Ushirikiano Unaotuwezesha Kuendelea Kuishi.”

© FAO/Richard Slaby Asilimia 75 ya mazao ya chakula ulimwenguni, kama vile apple, kahawa na blueberries, hutegemea uwepo wake kwa wachavushaji.

Kwa nini kuna Siku ya Nyuki Duniani?

Siku ya Nyuki Duniani imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka tangu 2018 kufuatia juhudi za Serikali ya Slovenia kwa kushirikiana na Apimondia, zilizowezesha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutangaza rasmi tarehe 20 Mei kuwa siku maalum ya kuenzi nyuki na wachavushaji wengine.

Tarehe hiyo ilichaguliwa kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Anton Janša, anayefahamika kama mmoja wa waanzilishi wa ufugaji nyuki wa kisasa. Janša alitoka katika familia ya wafugaji nyuki nchini Slovenia na alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya ufugaji nyuki barani Ulaya.

FAO imesema siku hiyo ni fursa muhimu kwa serikali, mashirika, watafiti, wakulima, wafugaji nyuki na wananchi duniani kuhamasisha hatua za kulinda wachavushaji pamoja na makazi yao.

Nyuki wana mchango mkubwa katika chakula chetu

Kwa mujibu wa FAO, zaidi ya asilimia 75 ya mazao ya chakula duniani hutegemea uchavushaji kwa kiwango fulani. Wachavushaji kama nyuki, vipepeo, ndege, nondo, mende na popo husaidia mimea kuzaliana na kuongeza uzalishaji wa mazao muhimu ya chakula.

FAO inaeleza kuwa matunda mengi, mboga, mbegu, karanga na mazao ya biashara kama kahawa, kakao na parachichi hutegemea uchavushaji ili kutoa mazao bora na mengi zaidi.

Shirika hilo limesisitiza kuwa dunia bila wachavushaji ingekuwa na upungufu mkubwa wa vyakula mbalimbali muhimu kwa afya ya binadamu.

Mbali na chakula, nyuki pia huchangia uzalishaji wa dawa, mafuta ya asili, nyuzi za kutengeneza mavazi pamoja na bidhaa nyingine nyingi zinazotumiwa katika maisha ya kila siku.

© Unsplash/Boris Smokrovic Nyuki wa magharibi hutoa tani milioni 1.6 za asali kwa mwaka.

Hatari zinazowakabili nyuki duniani

Pamoja na umuhimu huo mkubwa, FAO imeonya kuwa idadi ya nyuki na wachavushaji wengine inaendelea kupungua kwa kasi duniani kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu na mabadiliko ya mazingira.

Sababu zilizotajwa ni pamoja na:

· Matumizi makubwa ya viuatilifu na kemikali hatari
· Kilimo kisicho rafiki kwa mazingira
· Uharibifu wa makazi ya asili ya nyuki
· Mabadiliko ya matumizi ya ardhi
· Magonjwa na wadudu waharibifu
· Spishi vamizi kutoka maeneo mengine
· Athari za mabadiliko ya tabianchi

FAO imeonya kuwa kupungua kwa wachavushaji kunaweza kuhatarisha uzalishaji wa chakula, kuongeza uhaba wa lishe bora na kuathiri maisha ya mamilioni ya wakulima duniani.

Kaulimbiu ya 2026 yaangazia ushirikiano kati ya binadamu na nyuki

Kwa mujibu wa FAO, kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuonesha namna binadamu na nyuki wamekuwa wakishirikiana kwa maelfu ya miaka katika kusaidia maisha ya watu, kilimo na mazingira.

Shirika hilo linasema jamii nyingi duniani zimekuwa zikitegemea nyuki kwa chakula, kipato na hata utamaduni wao. Aidha, maadhimisho ya mwaka huu yataonesha maendeleo ya ufugaji nyuki katika tamaduni mbalimbali pamoja na mbinu bunifu za kuboresha afya ya nyuki na uzalishaji wa asali.

Kaulimbiu hiyo pia inaendana na Maadhimisho ya Kimataifa ya Mwaka wa Nyanda za Malisho na Wafugaji 2026 pamoja na Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima 2026, kwa kuonesha mchango wa ufugaji nyuki katika maisha ya vijijini na kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Maadhimisho rasmi ya 2026

Katika kuadhimisha Siku ya Nyuki Duniani 2026, FAO kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kimataifa wanafanya matukio maalum ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa nyuki.

Miongoni mwa matukio hayo ni Jukwaa la Tatu la Kimataifa la Ufugaji Nyuki Endelevu na Uchavushaji linalofanyika mjini Maribor nchini Slovenia tarehe 20 hadi 21 Mei. Jukwaa hilo linawakutanisha watunga sera, watafiti, wafugaji nyuki, wakulima, asasi za kiraia na sekta binafsi kujadili namna ya kuimarisha uhifadhi wa wachavushaji duniani.

FAO pia inaendelea kuhimiza kuanzishwa kwa Jukwaa la Kimataifa la Wachavushaji litakalosaidia kubadilishana maarifa, tafiti na uzoefu kuhusu bioanuwai, kilimo-ikolojia na uhifadhi wa wachavushaji.

© Unsplash/Camille Cox Takriban asilimia 35 ya wanyama wasio na uti wa mgongo, hasa nyuki na vipepeo, wanakabili hatari ya kutoweka duniani kote.

Ushauri kwa wakulima na wananchi

FAO imehimiza wakulima na wananchi wote kuchukua hatua rahisi lakini muhimu za kusaidia nyuki na wachavushaji wengine.

Hatua hizo ni pamoja na:

· Kupanda mimea ya kienyeji inayotoa maua mara kwa mara
· Kupunguza matumizi ya viuatilifu hatari
· Kuhifadhi maeneo ya asili ya wachavushaji
· Kuweka maji safi kwa ajili ya nyuki
· Kununua asali ya asili kutoka kwa wafugaji wa eneo husika
· Kuunga mkono kilimo kinacholinda mazingira

Shirika hilo limesema hatua hizo zinaweza kusaidia kuongeza idadi ya wachavushaji na kuimarisha uzalishaji endelevu wa chakula.

© FAO/Didor Sadulloev Mkulima Nyuki wa Tajik Anakagua asali ya Nyuki

Wito wa kulinda wachavushaji duniani

FAO imehitimisha kwa kusisitiza kuwa kulinda nyuki ni kulinda uzalishaji wa chakula, kipato cha wakulima, bioanuwai na afya ya sayari kwa ujumla.

Shirika hilo limetoa wito kwa serikali, mashirika na wananchi duniani kushirikiana katika kulinda wachavushaji wa asili na wanaofugwa ili kuhakikisha usalama wa chakula kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *