DAR ES SALAAM: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria anayeshughulikia masuala ya siasa, Balozi Dk Hannah Liko, ambapo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika masuala ya uhamiaji, fursa za ajira, usalama pamoja na masuala ya wakimbizi.

Akizungumza baada ya kikao hicho kilichofanyika Dar es Salaam leo, Ayoub amesema katika eneo la uhamiaji, pande zote mbili zimejadili mienendo ya watu wanaotoka Austria kuja Tanzania na Watanzania wanaokwenda Austria, ambapo Tanzania imeeleza kuwa iko tayari kuendelea kuwapokea raia wa Austria kwa mujibu wa sheria na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima ili kukuza uchumi na maendeleo ya nchi hizo mbili.

Kadhalika, viongozi hao walijadili umuhimu wa kuimarisha usalama wa mataifa yao kwa kushirikiana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa mtandao (cybercrime).

Aidha, wamekubaliana kubadilishana taarifa na uzoefu katika kukabiliana na makosa ya mtandaoni, ikiwemo matumizi mabaya ya teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence) yanayoweza kusababisha upotoshaji wa taarifa au kuharibu taswira za watu.

Vilevile Katika masuala ya wakimbizi, Mhe. Ayoub ameeelezea kuhusu hali ya wakimbizi nchini Tanzania na hatua zinazoendelea za kuwarejesha wakimbizi, hususan kutoka Burundi, kurejea makwao kwa hiari, jambo ambalo limepongezwa na upande wa Austria chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika masuala ya Uhamiaji, na Usalama kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *