DAR ES SALAAM: BANDARI ya Dar es Salaam imeendelea kuwa nguzo muhimu ya upatikanaji wa mafuta kwa nchi jirani ya Malawi, hatua inayochochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya mafuta katika Kituo cha Kurasini Oil Jet (KOJ-1), kilichopo katika bandarini hapo leo Machi 24, 2026, Waziri wa Nishati na Madini wa Malawi, Dk Jean Mathanga, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango mkubwa katika kuwezesha mtiririko wa mafuta kwenda nchini Malawi.

Amesema kuwa kutokana na Malawi kutokuwa na bandari, nchi hiyo inategemea kwa kiasi kikubwa miundombinu ya nchi jirani, hususan Tanzania, katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika.

Amebainisha kuwa ziara hiyo imelenga kujionea kwa vitendo namna mafuta yanavyopokelewa na kusimamiwa bandarini ili kuboresha mipango ya ununuzi na usambazaji wa mafuta nchini Malawi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), ambaye ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Petroli PBPA, Mhandisi Bruno Tarimo, amefafanua kuwa sehemu kubwa ya mafuta yanayoingia Malawi hupitia Tanzania kupitia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS), huku wakati mwingine nchi hiyo ikiagiza moja kwa moja kutoka kwa wazabuni wake.