
Waziri Mkuu wa Uhispania ametangaza kwamba vita vya sasa vya Marekani na Wazayuni katika Mashariki ya Kati ni “vibaya zaidi” kuliko vita vya Iraq mwaka 2003 na ni “janga kubwa,” na kusema: Utawala wa Kizayuni wa Israel unataka kurudia “uharibifu” uleule wa Gaza nchini Lebanon.
Gazeti la El Pais limemnukuu Pedro Sanchez akisema kuhusu mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran kwamba: “Hili ni janga kubwa.”
Sanchez ambaye alikuwa akizungumza katika kikao cha hadhara cha Bunge la nchi hiyo kutetea msimamo wa serikali yake wa “kupinga vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran”, amesema: Tangu Februari 28, “karibu vifo vya watu 2,000 vimethibitishwa, zaidi ya watu milioni nne wameyakimbia makazi yao nchini Iran na Lebanon, takriban euro bilioni 12 za pesa za umma zimetumika katika shughuli za kijeshi, utalii, biashara ya baharini na usafiri wa anga duniani vimepungua sana, na bei ya hidrokaboni na malighafi muhimu kwa utendaji kazi mzuri wa uchumi wa dunia pamoja na usalama wa chakula imeongezeka kwa kiasi kikubwa.”
“Na haya yote ni kwa ajili ya nini?”, amehoji Waziri Mkuu wa Uhispania kuhusu uchokozi usio na msingi dhidi ya Iran na kujibu: “Kudhoofisha sheria za kimataifa, kuvuruga utulivu Mashariki ya Kati, kuibua migogoro katika nchi za Iraq na Lebanon, na kuizika Gaza chini ya vifusi vya usahaulifu na kutojali.”
Amesisitiza kwamba vita vya sasa Mashariki ya Kati ni “vibaya zaidi” kuliko vita vya Iraq vya mwaka 2003.
Waziri Mkuu wa Uhispania amesema: Mashambulizi ya Marekani na Israel yalianza wakati Marekani ilikuwa na makubaliano ya nyuklia na Iran “mikononi mwake” lakini iliyatupilia mbali “bila kutoa maelezo, bila kuwafahamisha washirika, bila kuungwa mkono kisheria, na bila lengo maalumu.”