TIMU ya Taifa ya wachezaji wa tenesi kwa watu wenye ulemavu (Wheelchair Tennis) imeomba msaada wa Shilingi milioni 40 ili kufanikisha safari ya kushiriki mashindano ya kimataifa yatakayofanyika nchini Morocco kuanzia Machi 30 hadi Aprili 3, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kocha wa timu hiyo ambaye pia ni Katibu Riziki Salumu, amesema timu imejiandaa kikamilifu kushiriki mashindano hayo muhimu. Amesema jumla ya watu 10 wanatarajiwa kusafiri, wakiwemo wachezaji wanane, kiongozi mmoja pamoja na msaidizi wake.
Ameongeza kuwa ushiriki wao utasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa na kuwapa wachezaji fursa ya kupata ufadhili endapo watafanya vizuri. Salumu amesema gharama za safari hiyo ni Shilingi milioni 50, ambapo hadi sasa wamefanikiwa kukusanya Shilingi milioni 17, hivyo bado wanahitaji Shilingi milioni 40 ili kukamilisha maandalizi.
Kwa upande wake, nahodha wa timu hiyo, Vosta Isaya, amewaomba wadau, mashirika pamoja na Serikali kujitokeza kuisaidia timu hiyo ili iweze kushiriki mashindano hayo muhimu. Mchezaji wa timu hiyo, Pendo James, amesema maandalizi yalianza tangu Januari mwaka huu, huku akieleza kuwa mashindano hayo yamesogezwa mbele kutokana na mwezi wa Ramadhani.
Aidha, Jumanne Nasoro amesema mwaka jana timu ya wanawake ilipata udhamini na kushiriki mashindano hayo, lakini timu ya wanaume haikufanikiwa, hivyo mwaka huu wana matumaini makubwa ya kupata msaada. SOMA: Tennis yaipamba Hifadhi ya Serengeti
Wachezaji hao wamesisitiza kuwa kushindwa kushiriki mashindano hayo kunaweza kusababisha adhabu ya kutojumuishwa katika mashindano yajayo, wakibainisha kuwa michezo ni ajira na chanzo cha kipato hivyo wanahitaji kuungwa mkono ili kufanikisha ndoto zao.
