Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Haroun Kahena maarufu Inspector Haroun, amezungumza kuhusu mwenendo wa timu yake aipendayo, Simba SC, na kugusia masuala ya makocha, wachezaji, na hata mashabiki.

Akizungumza na Mwananchi, Inspector Haroun alianza na mabadiliko ya makocha yaliyofanywa na timu ya Simba kwa msimu huu. Alisema hilo limekuwa tatizo la muda mrefu ndani ya timu, huku akisisitiza kuwa kukosekana kwa uimara kumekuwa kikwazo kikubwa cha mafanikio.

“Timu yetu itambue imebadili makocha muda mrefu mno. Hili tatizo sio la walimu wala wachezaji; timu inatakiwa kukaa pamoja muda mrefu na kuwa imara,” alisema Inspector Haroun.

Pia, Inspector Haroun aliwakumbusha mashabiki wa Simba nyakati za mafanikio ya timu hiyo akiwataja baadhi ya mastaa walioitumikia kama Clatous Chama, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na wengine, akisisitiza kuwa mafanikio huja kwa uvumilivu na muendelezo wa kikosi.

Inspector Haroun aliendelea kusema kuwa timu imekuwa ikiyumba kwa muda mrefu, hali iliyosababisha hata kukosa mwelekeo uwanjani, akiwataka viongozi kuongeza umakini. Aliwatahadharisha pia baadhi ya mashabiki wanaotamani wapinzani wao wafungwe ili wao wanufaike, akisema hiyo si njia sahihi ya ushindani.

“Tumeyumba muda mwingi tukakosa hata pa kushika. Hii timu viongozi wanatakiwa kuitolea macho kweli kweli. Bora tuokote point zetu; kusubiri wengine wapoteze ni mtihani, kuna sehemu tulikosea hapo nyuma,” alisema Inspector Haroun.

Kuhusu benchi la ufundi, Inspector Haroun alimtetea kocha wa Simba, akisema si mbaya, ila ana misimamo yake ambayo wakati mwingine haieleweki kwa mashabiki. Hata hivyo, aliwataka mashabiki kuendelea kumpa muda na kumuunga mkono.

Akizungumzia mechi ya hivi karibuni kati ya Yanga na Azam, alisema Azam hawakuwa na ushindani mkubwa kwa Yanga, huku akiamini Simba wana uwezo wa kufanya vizuri zaidi wanapokutana na wapinzani hao.

Hata hivyo, Inspector Haroun aliwataka mashabiki kuwa na subira na imani, akisisitiza kuwa mbio za ubingwa bado zipo wazi. “Tuombe uzima, ligi bado ipo, lolote linaweza kutokea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *