Dar es Salaam. Kampuni ya Caps Limited ya Tanzania imeibuka kidedea katika anga za kimataifa baada ya kutwaa tuzo mbili za ubora katika shindano la SADC Annual Quality Awards lililofanyika usiku wa Machi 25, 2026 jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Katika shindano hilo lililoshirikisha kampuni na taasisi kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Caps Limited ilinyakua Tuzo ya Mtoa Huduma Bora wa Mwaka na kushika nafasi ya pili katika kipengele cha Kampuni Bora ya Mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Peter Marealle amesema ushindi huo ni uthibitisho wa juhudi za muda mrefu za kampuni katika kuzingatia viwango vya kimataifa vya utoaji huduma.

“Tunajivunia kuiwakilisha Tanzania kimataifa. Tumepimwa kwa viwango vya ubora wa huduma na tumefanikiwa kushinda, jambo linalothibitisha dhamira yetu ya kutoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa,” amesema Marealle.

Amesema mafanikio hayo yanaipa Caps Limited nafasi ya kutambulika zaidi kimataifa, huku yakifungua fursa kwa makampuni ya ndani kuaminiwa na wawekezaji na washirika wa nje.

Kwa mujibu wa Marealle, siri ya mafanikio hayo licha ya ushindani mkali ni uwazi katika utendaji, nidhamu ya kazi pamoja na kuzingatia taratibu za kimataifa katika utoaji wa huduma.

Ameongeza kuwa kampuni nyingi za kimataifa zinazoingia nchini huzingatia ubora wa huduma za wazawa, hivyo ushindi huo ni chachu kwa sekta binafsi kuongeza ubora na ushindani.

Caps Limited ni kampuni ya kizalendo inayojishughulisha na udhibiti wa wadudu waharibifu, utoaji wa huduma za vyoo vya kibiolojia na vya kukodisha, pamoja na usambazaji wa vimeng’enya kwa ajili ya uchakataji wa maji taka.

Marealle ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa mchango wao katika kuhakikisha huduma na bidhaa za ndani zinazingatia viwango vinavyotambulika kimataifa.

“Ushirikiano tulioupata kutoka serikalini umetuwezesha kufikia hatua hii. Bila msaada huo, ingekuwa vigumu kutambulika kimataifa,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja Ubora wa kampuni hiyo, Noela David Mkusu ameiomba Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kupunguza urasimu na mzigo wa kodi unaokwamisha ukuaji wa sekta binafsi.

Amesema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, hivyo ni muhimu kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha ushindani wa kimataifa.

Mkusu pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kukuza uchumi, akisema ushindi huo ni wa Watanzania wote.

“Lengo letu ni kuendelea kuboresha huduma na hatimaye kushinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha Kampuni Bora ya Mwaka kwa utoaji huduma,” amesema.

Mbali na mafanikio hayo, Caps Limited imeendelea kujizolea tuzo mbalimbali za ubora katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo kushinda Tuzo za Ubora za Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2022 katika sekta ya huduma kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

Mwaka 2024, kampuni hiyo ilinyakua tuzo mbili zaidi, ikiwemo kampuni Bora ya Mwaka na Mtoa Huduma Bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *