
Uchunguzi wa Gazeti la The Guardian, uliochapishwa Machi 25, unaangazia ukosefu wa mashtaka kufuatia mamia ya vifo katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ambapo mashambulizi dhidi ya vijiji vya Wapalestina yanaendelea.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Ramallah, Alice Moreno
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Gazeti la Uingereza la The Guardian, zaidi ya Wapalestina elfu moja wameuawa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa tangu mwaka 2020, na hakuna mhalifu, mlowezi au mwanajeshi wa Israel, aliyeshtakiwa. Katika kivuli cha vita vya kikanda, mashambulizi yanayolenga vijiji vya Wapalestina hutokea kila siku.
Karibu na Nablus, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kaskazini, hema liliwekwa mapema asubuhi ya leo na walowezi karibu na kijiji cha Beyt Imrin. “Hapo, unaweza kuona hema, unaweza kuona bendera ya Israel kati ya miti miwili,” anaelezea Bassam, mwandishi wa habari wa Palestina, akionyesha shamba lake mwenyewe, lililo karibu na ambalo sasa halifikiki. “Nina wasiwasi, bila shaka, ni ardhi yangu, ni nyumba yangu,” anakiri.
Mvutano karibu na kituo cha jeshi la Israel
Karibu mita mia moja kutoka kituo hiki, kundi la Wapalestina linakamatwa. Wakiwa na fimbo, walikuwa wamewakabili walowezi dakika chache mapema. “Hii si mara ya kwanza kutushambulia. Walichukua kondoo wetu, matrekta yetu. Hawakuacha chochote… Hatuwezi kulala tena, tunakaa macho saa 24 kwa siku. Wanatushambulia kwa fimbo,” anashuhudia Tarek.
Licha ya kuwepo kwa baadhi ya walowezi wakiwa na bunduki za kivita, wakazi kadhaa wanasema wako tayari kurudi katika eneo hilo ili kupata sehemu zao za ardhi. “Walowezi wako pale pale, wamejipanga katika ardhi yetu! Jeshi lilikuja. Niliwaomba, ‘Wafukuzeni kutoka katika ardhi yetu.’ Walijibu, ‘Hapana, wanabaki,'” anaripoti mkazi mmoja. Mwingine anaongeza, “Tunakusanyika ili kurudi na kufanya jambo, kwa sababu hakuna mtu mwingine anayeweza kuchukuwa hatua kwa dhulma hii.”
Wakati timu ya RFI ilipoondoka katika eneo hilo, Mpalestina aliyebaki hapo anasema kwa simu kwamba walowezi walifyatua risasi za moto, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa. Jeshi la Israel lilipowasiliana na RFI, lilisema kwamba linajua kuhusu kuwekwa kwa kituo hicho na kuahidi kukihamisha, bila kutaja muda maalum.