
Kampuni ya Airtel Africa kwa kushirikiana na SpaceX, wametangaza kufanikiwa kwa majaribio ya huduma za data na ujumbe mfupi (SMS) kupitia teknolojia ya Starlink Mobile nchini Kenya.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa muhimu katika kufungua njia ya upatikanaji wa mawasiliano ya satelaiti moja kwa moja kwenye simu za mkononi kwa mamilioni ya wananchi katika nchi 14 ambako Airtel inatoa huduma barani Afrika.
Majaribio hayo yalifanyika katika maeneo yasiyo na mtandao wa kawaida wa simu, ambapo minara ya mawasiliano haikuwa na mawimbi.
Kupitia teknolojia hiyo, simu janja za 4G ziliweza kuunganishwa moja kwa moja na mtandao wa satelaiti zaidi ya 650 zilizopo angani, hivyo kuwezesha mawasiliano kuendelea hata katika maeneo ya mbali.
Katika majaribio hayo, watumiaji waliweza kutumia huduma za data nyepesi ikiwemo kutuma ujumbe kupitia WhatsApp, kutumia ramani, Facebook Messenger pamoja na kufanya miamala ya kifedha kupitia Airtel App.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa vitendo wa ushirikiano kati ya kampuni hiyo na SpaceX.
Alisema majaribio yaliyofanyika Kenya yanaonyesha dhamira ya kupanua huduma za mawasiliano kwa wananchi wengi zaidi, hasa walioko katika maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya kawaida.
“Kwa kuunganisha teknolojia ya Starlink Mobile, tunahakikisha wateja wetu wanaendelea kuwasiliana hata wanapokuwa nje ya maeneo yenye mtandao wa kawaida,” alisema Taldar.
Baada ya mafanikio hayo, Airtel Africa na SpaceX wanatarajia kupanua huduma hiyo katika nchi zote 14 wanazofanya kazi, kulingana na vibali vya mamlaka za mawasiliano za kila nchi.
Aidha, kampuni hizo zimeeleza kuwa zinapanga kuanzisha huduma za kupiga simu kwa sauti pamoja na intaneti yenye kasi zaidi kupitia toleo la Starlink Mobile V2, litakalowezesha watumiaji kupata huduma za mawasiliano moja kwa moja kwenye simu bila kutegemea minara ya kawaida.