
Iran imeuarifu rasmi Umoja wa Mataifa kuhusu ripoti za vyombo vya habari zinazofichua mipango ya hila ya Marekani na Israel ya kuwaua maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu, akiwemo Spika wa Bunge Mohammad Baqer Qalibaf na Waziri wa Mambo ya Nje Sayyid Abbas Araghchi, ikielezea vitisho hivyo kama mfano wazi wa ugaidi wa serikali na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Katika barua rasmi aliyoitumwa jana kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Baraza la Usalama, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeed Iravani, alieleza wasiwasi mkubwa kuhusu njama za mauaji ya viongozi wa ngazi za juu wa Iran zinazopangwa na Marekani na Israel.
“Ninapenda kukujulisha haraka Mheshimiwa na wanachama wa Baraza la Usalama kuhusu ripoti zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari,” amesema Iravani.
“Ripoti hizi zinaonyesha kwamba Marekani na utawala wa Israel wamewatambua na kuwateua maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akiwemo Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), Bw. Mohammad Baqer Qalibaf, na Waziri wa Mambo ya Nje, Bw. Sayyid Abbas Araghchi, kama walengwa wa mauaji.”
Balozi wa Iran UN amesisitiza kwamba ripoti hizo zinaashiria mfumo wa uendeshaji unaolenga kuwaua maafisa wakuu wa kisiasa wa Iran na kuongeza: Sera hii ya jinai imetekelezwa kimfumo tangu kuanza kwa uchokozi usio na sababu wa Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28, ambao ulizinduliwa kwa mauaji ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na maafisa wengine kadhaa wa ngazi za juu.
“Sera kama hiyo inaonyesha wazi ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa” imesema sehemu ya barua ya Iravani kwa Baraza la Usalama la UN na kuongeza: Vitisho hivi ni matokeo ya “mawazo ya uhalifu” na vinatia wasiwasi mkubwa.”
Amesema: Utumiaji wa istilahi ya ‘orodha za mauaji’ unapaswa kuonekana kama dhihirisho lingine la vitendo vile vile vya kigaidi vilivyoanzisha vita vya kihalifu dhidi ya Iran na hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya raia elfu tatu.”
Iravani amesisitiza kwamba sera iliyopangwa mapema ya kuwaua maafisa wa ngazi za juu wa nchi huru mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni ukiukwaji mkubwa wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, pamoja na uvunjaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu – ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi – na sheria za kimataifa za kibinadamu.