MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Stephen Wasira amewaonya wanachama walioanza harakati za kusaka urais mwaka 2030 akisema muda wa kufanya hivyo bado haujawadia.
Wasira amesisitiza kuwa kuanza mapema harakati kunakiuka kanuni, miongozo na utaratibu wa Chama. “Kuanzisha harakati za uongozi kabla ya wakati kunaweza kugawa Chama badala ya kuimarisha umoja wake, hivyo ni jambo linalopaswa kukemewa,” alisema Wasira.

Kauli hiyo ameitoa mjini Bunda, Mkoa wa Mara, alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ofisi za CCM Wilaya ya Bunda, ambazo zilichomwa moto katika vurugu za Oktoba 29, 2025. Ameongeza kuwa ndani ya Chama kuna kundi la wanachama ambao hawana kazi za msingi za chama zaidi ya kujihusisha na makundi ya kisiasa.
Wasira amesema hivi sasa kuna baadhi ya wanachama wameanza kujipanga kuanzia ngazi za kata jambo ambalo linaweza kusababisha mgawanyiko ndani ya CCM kwani kila mmoja anataka wafuasi wake badala ya kuimarisha umoja.

Wasira amehoji uhalali wa baadhi ya wanachama kuanza kujitangaza mapema kuwania urais wa 2030, akisema hakuna anayeweza kujihakikishia uwepo wake hadi wakati huo. “Unazungumziaje urais wa 2030 leo, wakati hata hujui kama utakuwepo? Hiyo ni kama kumjaribu Mungu. Wakati huu tunapaswa kujikita kwenye kazi za kujenga Chama na nchi,” alisisitiza.
Aidha, amewaonya baadhi ya watu kutumia fedha kushawishi wanachama maskini kuungwa mkono akieleza kuwa hali hiyo ni hatari na inaweza kuharibu maadili ya Chama. SOMA: ‘Muwe mabalozi wa amani’