MWANAUME mmoja anayefahamika kwa jina la Bunzali Jidola (30), mkazi wa Kijiji cha Imalanguzu, Kata ya Mwamakona, Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, anadaiwa kumuua mtoto wake mchanga wa miezi miwili,
Doricas Bunzali anadaiwa kumchinja mtoto wake kwa kutumia kitu chenye ncha kali, kisha kumjeruhi vibaya mke wake Geni Ndaki (24) kabla ya kutokomea kusikojulikana. Tukio hilo limetokea Machi 25, 2026, majira ya saa 3:00 usiku katika Kitongoji cha Ibindo, kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Richard Abwao.
Mke aliyejeruhiwa alikimbizwa Hospitali ya Nkinga kwa matibabu baada ya kupatiwa fomu ya PF3 ambapo hali yake imeelezwa kuwa ni mbaya. Juhudi za kumtafuta mtuhumiwa zilihusisha vikosi vya kijamii vya ulinzi na usalama ambao walimkuta akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka kwenye nguzo ya umeme ya TANESCO katika eneo hilo.
Taarifa ya polisi inabainisha kuwa chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi, kwani mtuhumiwa alihisi mtoto si wake. Pia inadaiwa alitekeleza kitendo hicho siku mbili tu baada ya kurejea kutoka kwenye machimbo ya madini ya Bulangamilwa, Kata ya Choma, Wilaya ya Igunga, ambapo alikuwa akifanya shughuli za uchimbaji tangu Agosti 2025. SOMA: Polisi wamkamata kijana kwa mauaji
