Wajumbe wengi walitoka nje ya ukumbi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kama ishara ya kupinga hotuba ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, wakati wa kikao cha 80 cha UNGA.
Netanyahu, ambaye kwa sasa anakabiliwa na hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutokana na uhalifu wa kivita, alitumia hotuba yake siku ya Ijumaa kutetea vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.
Mtawala huyo katili alikosoa msimamo wa mataifa mbalimbali wanachama na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa utawala wake lazima “ukamilishe kazi” katika eneo la Palestina lililozingirwa.
Kauli zake zilikuja baada ya viongozi kadhaa wa dunia kutoa hotuba kali katika Umoja wa Mataifa dhidi ya Israel na kuitaka isitishe vita vyake vya kikatili dhidi ya Gaza.
Israel inakabiliwa na hali ya kutengwa isiyokuwa ya kawaida huku mahinikizo ya kidiplomasia, kitamaduni, na kiuchumi yakiongezeka.
Kuondokakwa wajumbe kwa wingi katika ukumbi wakati wa hotuba ya Netanyahu ni ishara ya wazi ya hasira ya kimataifa dhidi ya vita vya Gaza, hali ambayo sasa inaonekana katika hatua rasmi za kutambua taifa la Palestina na kampeni za kususia utawala wa Israel.
Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, imesema kuwa hatua ya wajumbe wa mataifa wanachama wa UN kuondoka kabla ya Netanyahu kuzungumza ni ishara ya kutengwa kwa Israel kimataifa kutokana na vita vya Gaza.
Taher al-Nunu, mshauri wa vyombo vya habari wa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas: “Ususiaji wa hotuba ya Netanyahu ni miongoni mwa dalili za kutengwa kwa Israel kutokana vita vya Gaza.”
Katika hotuba yake, Netanyahu alionyesha kiburi na ukaidi kwa kutangaza kuwa anapinga hatua ya mataifa ya Magharibi na Ulaya kutambua taifa la Palestina, na akaapa kuwa Israel itaendeleza ukatili na mauaji dhidi ya Wapalestina Gaza huku akidai kuwa lengo ni kuangamiza Hamas.

Hata washirika wa jadi wa Israeli wameanza kukosoa kimaonyesho vita vya Gaza, huku nchi za Uingereza, Ufaransa, Australia na Kanada zikiwa miongoni mwa waliotangaza kutambua taifa la Palestina hivi karibuni.
Kwa kutumia hoja ya zamani, Netanyahu alidai kuwa kutambua taifa la Palestina ni kwa faida ya harakati kama Hamas—japo mataifa 157 tayari yametambua rasmi taifa la Palestina.
Netanyahu amedai hakuna mauaji ya kimbari Gaza. Madai hayo yanakuja licha ya ripoti ya hivi karibuni ya tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu kuthibitisha kuwa Israel imefanya mauaji ya kimbari Gaza. Ripoti hiyo imeungwa mkono na wataalamu huru wa haki za binadamu na wasomi mbalimbali.
Mnamo Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC ilitoa hati za kukamatwa dhidi ya Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita, Yoav Gallant, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu Gaza.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya Wapalestina 65,500 wameuawa, na zaidi ya 167,500 kujeruhiwa tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari mnamo Oktoba 2023. Waathirika wengi wa mashambulizi ya Israeli bado wamekwama chini ya vifusi na mitaani.