SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Mitaji (UNCDF) limesema kuwa linaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.
Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa UNCDF, Peter Malika amesema baada ya shirika hilo kutoa majiko ya kisasa katika shule ya Msingi Bunge jijini Dar es Salaam kuunga mkono matumizi ya nishati safi katika taasisi za umma.
Amesema msaada huo ni sehemu ya mradi CookFund unaohusisha usambazaji wa nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).

Amesema kupitia mradi huo jumla ya sh bilioni 26 zimetolewa kama mikopo kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) 102 zinazojihusisha na biashara ya nishati safi ya kupikia katika wilaya 14 za Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza.
Malika amesema pia kuwa wanafunzi wapatao 62,000 katika shule mbalimbali nchini Tanzania wamenufaika na mpango huo, huku UNCDF ikilenga kufikia taasisi 147 za umma ifikapo Septemba mwaka huu.
“Malengo yetu ni kuunga mkono ajenda ya nishati safi inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha asilimia zaidi ya 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi hapa nchini”, amesema Malika.
Akiongea wakati wa kupokea msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Bunge, Leonida Mlekule ameishukuru UNCDF kwa msaada huo wa kuhamaisha matumizi ya nishati safi na kuunga mkono mpango wa matumizi ya nishati safi.

Amesema nishati safi mbali na kuli da mazingira pia inapunguza gharama kwani matumizi ya mkaa yamekuwa yanaigharimu shule hiyo zaidi ya milioni mbili, lakini majiko hayo yataokoa takribani sh milioni moja.
Naibu Waziri wa Nishati , Salome Makamba ameishukuru UNCDF kwa msaada huo na kuahidi ushirikiano zaidi katika kufanikisha ajenda hiyo ya matumizi ya nishati safi hapa nchini.
Salome amesema kuwa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi zinazolisha watu zaidi ya 250 zinatakiwa kuwa na majiko ya kisasa yenye matumizi ya niashati mbadala ya kupikia katika kulinda afya na mazingira.