JESHI la Polisi mkoani Geita limethibitisha kuwa hakuna madhara ya binadamu yaliyotokana na ajali ya kutitia kwa maduara manne ya uchimbaji madini katika mgodi wa Msasa, wilayani Bukombe mkoani humo.
Tukio hilo lilitokea Machi 29, 2026 majira ya saa nne asubuhi katika eneo la maduara ya uchimbaji yanayofanyiwa ukarabati katika mgodi huo, uliopo Kata ya Runzewe Magharibi. Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo, amethibitisha taarifa hiyo baada ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kukamilisha zoezi la uchunguzi.
Amesema uchunguzi umebaini kuwa wakati wa tukio hilo hakuna shughuli za uchimbaji zilizokuwa zinaendelea, kwani tahadhari ilikuwa imeshatolewa baada ya kuwepo kwa dalili za hatari. “Kwa kushirikiana na uongozi wa mgodi, tulihakikisha tunalifukua eneo lote lililotitia ili kujiridhisha kuwa hakuna madhara yaliyotokea,” alisema.
Ameongeza kuwa baada ya zoezi la ufukuaji kukamilika, baadhi ya vifaa vya uchimbaji vilikutwa chini ya ardhi, lakini hakukuwa na mwili wala viashiria vya kuwepo kwa binadamu. “Uvumi uliosambaa kwamba watu zaidi ya 200 wamepoteza maisha si wa kweli.

Mgodi umetitia, lakini hakuna madhara kwa binadamu,” alisema. Amewataka wananchi kuepuka kusambaza taarifa za uzushi na badala yake kutoa taarifa sahihi kupitia vyombo husika. Ameonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayesambaza taarifa za uongo zinazoweza kusababisha taharuki.“Mkoa wa Geita ni salama na mgodi wa Msasa uko salama.
Changamoto kama hizi ni za kawaida katika shughuli za uchimbaji,” alisema. Amesema pia tahadhari, maelekezo na mafunzo ya usalama yametolewa kwa wachimbaji wadogo, hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika, ili kuepusha madhara. SOMA: Mgodi wachangia bil 1.29/- serikalini miaka mitatu
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Geita, Keneth Mwakasitu, amesema uchunguzi umefanyika kwa umakini mkubwa kubaini hali halisi ya tukio hilo. Amesema hadi kufikia saa mbili usiku wa siku ya tukio, hakukuwa na madhara ya binadamu yaliyobainika. “Kazi ya utafutaji na uokoaji imefanyika vizuri, na taarifa zozote zinazoendelea kusambazwa mitandaoni kuhusu vifo ni za uongo,” alisema.