Lindi. Chama Kikuu cha Ushirika Lindi mwambao kimefanya mkutano wake wa tisa wa mwaka wenye lengo la kujadili maendeleo ya chama hicho pamoja na maandalizi ya kuelekea kwenye msimu wa zao la ufuta la mwaka 2026/2027
Akizungumza Jana Jumapili Machi 29, 2026 Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, amesema kuwa msimu wa mwaka 2025/2026 zao la ufuta katika chama kikuu cha ushirika Lindi mwambao iliingiza Sh133 bilioni, korosho iliingiza Sh101 bilioni huku mbaazi ikiingiza Sh3 bilioni, ambapo pia amewataka wakulima kuongeza juhudi ya kuzingatia ubora wa mazao hayo ili msimu wa mauzo unapofika waweze kupata bei nzuri.
Aidha amekitaka chama kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao kuweka mipango madhubuti katika kuleta maendeleo na iwe chachu katika kusimamia misingi ya ushirika pamoja na kusimamia vyama vya msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva, akizungumza na viongozi wa Amcos kwenye mkutano wa tisa wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao lengo ni kujadili mafanikio na maendeleo yaliyopatikana katika msimu wa 2025/2026 na kuelekea msimu wa ufuta wa 20262027. Picha na Bahati Mwatesa
“Mazao ya mbaazi ,ufuta na korosho yameungiza fedha nyingi sana kwenye chama chetu,hivyo basi niwaombe viongozi wa Amcos kujitahidi kwenda kuwashauri wakulima wetu wazingatie ubora wa mazao pamoja na usafi ili minada inapoanza tuweze kupata bei nzuri na soko bora kwa msimu unaokuja.amesema Mwanziva.
Aidha Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Lindi Keneth Shemdoe amesema kuwa hadi sasa mkoa huo umesajili vyama vya ushirika 193.
Amesema pia mafanikio yaliyopatikana yanatokana na juhudi za pamoja, ikiwemo ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhi mazao, ununuzi wa vyombo vya usafiri, uwekezaji kupitia hisa za wanachama, matumizi ya mizani za kidigitali, pamoja na uwekezaji katika benki za ushirika.
“Muhimu ni kuendelea kuhamasisha uwekezaji, kuongeza thamani ya mazao, na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi kupitia sekta ya ushirika, ambayo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi mkoani Lindi.”amesema Shemdoe
Naye mwenyekiti wa chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao kinachojumuisha Wilaya ya Lindi, Halmshauri ya Mtama pamoja na Wilaya Kilwa Ismail Nalinga amesema kuwa chama hicho kimeweza kupata mafanikio makubwa kwa kuingiza fedha nyingi kwenye mazao ya korosho,ufuta na mbaazi.
Pikipiki 32zilizotolewa na Lindi Mwambao kwa viongozi wake wa Amcos lengo ni kurahisisha upataikanaji wa huduma kwa wakulima wao
Pia chama hicho kimeweza kutoa pikipiki 32 kwa vyama vya msingi (Amcos) zenye thamani ya Sh112milioni ili kuweza kuwasaidia viongozi wa Amcos kuwafikia wakulima wao kwa urahisi katika kufuatilia ubora wa mazao.
“Viongozi wetu wa Amcos wamekuwa wakitoa elimu za marakwamara kwa wakulima wetu ikiwemo ubora wa mazao na kufikia mafanikio haya tuliyonayo sasa ambapo kwa msimu uliopita tumeingiza fedha nyingi katika mazao ya ufuta, mbaazi na korosho.”amesema Nalinga.
Hatahivyo Makamu Mwenyekiti kutoka chama cha msingi Nangaru Rashidi Masoud amesema kuwa pikipiki zilizotolewa zitaleta manufaa makubwa katika ufuatiliaji kwa wakulima hasa kutoa elimu za marakwamara kuhusiana na uwaandaji wa mazao kabla ya kuingia kwenye minada pamoja na kufanya malipo kwa wakati kwa wakulima wao.