RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kusisitiza uzingatiaji wa sheria katika shughuli zake ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma.
Rais Samia ameyasema hayo Ikulu, Dar es Salaam, alipokuwa akipokea taarifa za ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Amesema Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kuzingatia masharti ya ununuzi wa umma pamoja na uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma yanazingatiwa kwa mujibu wa sheria. “Naomba tujikumbushe kuwa uwajibikaji sio chaguo bali ni wajibu nataka kuwajibika au sitaki hapana,” alisema.

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya fedha za umma hutumika katika manunuzi ya serikali. Katika ripoti hizo, Rais Samia alibainisha kuwepo kwa mapungufu katika mifumo ya mawasiliano ya ndani, hali inayokwamisha ufuatiliaji wa taarifa. SOMA: Rais Samia apokea mapendekezo 284 maboresho mifumo ya kodi
Kutokana na hilo, amezielekeza wizara tatu ambazo ni Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Fedha na Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushirikiana kuimarisha matumizi ya mfumo wa NeST ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika taasisi za serikali. “Kwa kazi ya kufanya mifumo isomane ni endelevu kuendelea kusimamia ipasavyo kuboresha mifumo hiyo ili kuimarisha uwajibikaji na kupunguza mianya ya ubadhirifu wa fedha za serikali,” alisema Rais Samia.