Nchini Burundi, bado taarifa za maafa yaliyotokana na mlipuko wa ghala la silaha jijini Bujumbura, zimekuwa finyu, ripoti mbalimbali zikithibitisha watu kadhaa kupoteza maisha.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Milipuko hiyo ilishuhudiwa Jumanne jioni kwenye ghala kuu la silaha la Jeshi la Ulinzi la Burundi (FDNB) huko Musaga, kitongoji cha kusini mwa Bujumbura, msemaji wa jeshi akisema tukio hilo ni ajali ya umeme.
Afisa mmoja wa ngazi wa juu wa jeshi amesema ni vigumu kwa sasa kujua idadi ya vifo, lakini makumi kwa makumi wameuawa na mamia au hata maelfu kujeruhiwa.
Kituo hiki cha Musaga kiko katika eneo lenye watu wengi na kiko karibu na kambi nyingine ya kijeshi, kambi ya Muha, na gereza kuu la Mpimba.
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, katika ujumbe kwenye X, ameonyesha kusikitishwa na tukio hili, huku mamlaka zikiwaomna raia kuripoti kwa njia ya simu, silaha ambazo hazijalipuka.
Katika mitandao ya kijamii, machapisho kadhaa yameonyesha watoto wakitafutwa na wazazi wao baada ya kupotea njia wakati wakitoroka.