Chanzo cha picha, Reuters
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo
linatarajiwa kupigia kura rasimu ya azimio lililowasilishwa na Bahrain kuhusu
kulinda meli za kibiashara ndani na karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz.
China, ambayo ina nguvu ya kura ya turufu, inapinga
mpango wowote wa kutumia nguvu.
Bei ya mafuta imepanda kwa kasi tangu Marekani na
Israel zilipoanzisha mashambulizi dhidi ya Iran mwishoni mwa mwezi Februari, na
hivyo kuzua mzozo ambao sasa umedumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na kusababishwa kuufungwa
kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Wanadiplomasia walisema Bahrain, ambayo kwa sasa ni
mwenyekiti wa Baraza la Usalama lenye wanachama 15, imekamilisha rasimu ya
azimio lililoonekana na Reuters linaloidhinisha matumizi ya “njia zote
muhimu za kujihami” kulinda meli za kibiashara.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain Abdullatif bin
Rashid Al Zayani ameliambia baraza hilo, “Tunatazamia kupata msimamo mmoja
kutoka kwa baraza hili tukufu wakati wa upigaji kura utakaofanyika kesho(Ijumaa),
kuhusu rasimu ya azimio hilo” Mungu akipenda.
Hapo awali Bahrain ilikuwa imeondoa pendekezo la
utekelezaji wa sheria katika jaribio la kuzuia pingamizi kutoka kwa nchi
zingine, haswa Urusi na China.
Rasimu ya azimio inaidhinisha kuchukuliwa kwa hatua
hizi “kwa muda wa angalau miezi sita … na hadi Baraza litakapoamua
vinginevyo.”
Hata hivyo, Fu Cong, mwakilishi wa China katika
Umoja wa Mataifa, aliweka wazi katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama kwamba
Beijing inapinga kuidhinisha nchi wanachama kutumia nguvu.