DAR City na Petro de Luanda ya Angola zinatarajiwa kuonyeshana kazi katika mechi ya Ligi ya Kikapu ya Afrika (BAL) inayotazamiwa kutoa mwelekeo wa mabingwa wa Ligi ya Kikapu Dar es Salaam (BDL) kufuzu hatua nane bora ya mashindan hayo makubwa barani Afrika.

Mchezo huo unatarajiwa kushuhudiwa na mashabiki wengi, ambapo utafanyika katika uwanja wa ndani wa SunBet Arena mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Dar City itaingia uwanjani na kumbukumbu ya kufungwa na Al Ahly Ly kwa pointi 118-97 juzi, ilhali Petro de Luanda  ikipambana kushinda mchezo ili ipate nafasi ya kuwa moja ya timu nne zitakazocheza hatua ya mtoano BAL.

Dar City katika mchezo wa kwanza iliishinda Johannesburg Giants kwa pointi 100-70, kisha ikaifunga Nairobi City Thunder kwa pointi 90-85, na mchezo wa tatu ikafungwa na Al Ahly Ly kwa pointi 118-97.

Petro de Luanda iliifunga Al Ahly Ly kwa pointi 104-90, kisha ikafungwa na RSSB Tigers kutoka Rwanda kwa pointi 82-78. Inaonyesha kuwa mchezo huo utakuwa mgumu sana kutokana na kila timu kuhitaji ushindi kwa lengo la kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwa kwenye nafasi nne za juu.

Wachezaji nyota wa timu ya Dar City wanaotarajiwa kuwepo leo ni pamoja na Hasheem Thabeet, Nisre Zouzoua, David Michineau, Daniel Foster na Atiki Atiki.

Kwa upande wa timu ya Petro de Luanda, wanaotarajiwa kuwepo ni pamoja na Sofian Hamad, Childe Dundao na Milton Valent.

Dar City inatarajia kucheza tena mchezo wake wa tano kesho (Jumamosi) dhidi ya timu ya RSSB Tigers ya Rwanda. Timu hiyo inafundishwa na Mtanzania Henry Mwinuka, aliyewahi kuifundisha timu ya Dar City.

DAR CITY VS AL AHLY LY

Katika mchezo wake na Dar City, timu ya Al Ahly Ly ilifanikiwa kukamata eneo lote la uwanja, hali iliyofanya Dar City ishindwe kutegua mfumo wao mapema.

Kwenye michezo yake miwili iliyocheza, ilifungwa na timu ya RSSB Tigers kutoka Rwanda kwa pointi 52-47, ikafungwa tena na Petro de Luanda kutoka Angola kwa pointi 104-90, na mchezo wa tatu ikaifunga Dar City kwa pointi 118-97.

Katika mchezo huo, Majok Deng kutoka timu ya Al Ahly Ly alifunga pointi 22 kwa dakika 28:30 alizocheza, akifuatiwa na Jo Lual-Acuil aliyefunga pointi 20.

Kwa upande wa Dar City, alikuwa ni Michael Foster aliyefunga pointi 37 kutokana na dakika 39:60 alizocheza, akifuatiwa na David Michineau aliyefunga pointi 20 kutokana na dakika 39:60 alizocheza.

DAR CITY, CITY THUNDER KAMA DABI

Mchezo kati ya timu ya Dar City na Nairobi City Thunder ndiyo uliovutia katika Ligi ya Kikapu ya Afrika (BAL).

Kivutio cha mchezo huo kilitokana na ushindani mkubwa ulioonyeshwa na timu zote, hali iliyofanya wapenzi waliofurika katika uwanja wa ndani wa SunBet Arena, Pretoria, Afrika Kusini, washindwe kutabiri timu itakayoshinda.

Katika mchezo huo, wachezaji wa timu zote mbili walicheza kwa kasi katika robo zote nne, jambo lililofanya wapenzi wa timu zote kushangilia muda wote.

Kwa upande wa timu ya Dar City, waliovutia ni pamoja na Hasheem Thabeet, Nisre Zouzoua, Michael Foster na Atiki Ally Atiki. Kwa upande wa timu ya Nairobi City Thunder, waliovutia ni Tylor Ongwae, Ariel Okall, Jawachi Joseph na Phillips Adera.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *