KIUNGO mkabaji wa timu ya KMKM, Imran Mohammed Abdalla ‘Jaba’ amesema kati ya msimu ambao hawezi kuusahau ni huu wa 2025-2026 kwa jinsi timu hiyo ilivyopitia kwenye nyakati ngumu za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Amesema, KMKM ilianza msimu kwa kusuasua na kukaa kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja jambo ambalo lilimyima amani na furaha wakati wote.

Jaba amesema, baada ya timu kufanya mabadiliko ya bechi la ufundi na uongozi kwa ujumla, sasa imerudi kwenye ushindani wa ligi hiyo.

“Katika kipindi kigumu cha timu ilichopitia nimejifunza vitu vingi ambavyo vimenifanya kukua kiakili kwani nilikuwa sipati usingizi na kukosa raha kabisa kutokana na matokeo mabaya tuliyokuwa tunapata,” amesema Jaba.

Kiungo huyo, amesema jambo ambalo lilikuwa likimuumiza zaidi kuwa wanacheza vizuri lakini hawapati matokeo wanayoyataka.

Amesema, kwasasa wanashukuru timu imepata muunganiko mzuri na wameweza kupata matokeo mazuri kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo hadi kuondoka kwenye mstari wa kushuka daraja. Mbali na hilo, Jaba amesema timu hiyo ina lengo la kutetea ubingwa wa Kombe la FA msimu huu.

“Lengo ni kutetea ubingwa wa Kombe la FA na kumaliza ligi tukiwa katika nne bora au tatu bora, lakini hata nafasi ya kuwa mabingwa tunayo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *