BEKI wa kushoto wa Bigman FC, Adeyum Saleh amesema licha ya mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho msimu huu, bado wana fursa ya kumaliza nafasi tano za juu katika msimamo wa Ligi ya Championship, licha ya ushindani wa wapinzani wao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Adeyum amesema malengo ya timu hiyo yalikuwa ni kumaliza nafasi ya nne na kucheza mechi za ‘Play-Off’, kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu, ingawa, kwa mwenendo na ushindani ulivyo itakuwa ni bahati kutimiza hilo.

“Hatujakata tamaa kwa sababu mechi tisa zilizobakia lolote linaweza kutokea, kwetu sisi wachezaji tutaendelea kupambana hadi mwishoni ili tujue hatima yetu, ushindani ni mkubwa sana kutokana na mahitaji ya kila mmoja wetu,” amesema Adeyum.

Nyota huyo aliyewahi kuwika na timu mbalimbali zikiwemo Yanga, Coastal Union, Stand United, Kagera Sugar na Dodoma Jiji, amesema hadi sasa wako katika nafasi nzuri ya kujihakikishia kubaki Championship, japo wataendelea pia kupambana.

“Nafasi tuliyopo inatupa mwanga wa kutuhakikishia tuna uwezo wa kubakia Championship kwa msimu ujao kutokana na pointi tulizonazo, mechi hizi za mwishoni ni ngumu kutokana na mahitaji ya kila timu hivyo, ni lazima tuongeze umakini mkubwa.”

Bigman zamani ikifahamika kwa jina la Mwadui FC, katika Ligi ya Championship msimu huu iko nafasi ya saba na pointi 27, baada ya kikosi hicho kushinda mechi saba, kikitoka sare sita na kupoteza nane, huku ikifunga mabao 19 na kuruhusu 20.

Licha ya Adeyum kucheza beki, ila nyota huyo ameonyesha kiwango kizuri msimu huu na anashika nafasi ya pili kwa wachezaji wa Bigman waliofunga mabao mengi, akiwa na manne, nyuma ya Mnigeria Collins Kelvin Nwobodo mwenye matano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *