WAKATI Gunners FC ikijiandaa na mechi ya Ligi ya Championship dhidi ya Mbuni FC ya Arusha itakayopigwa Kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, Aprili 18, 2026, kocha wa timu hiyo, Mathias Wandiba amesema anafanyia kazi maeneo mawili tu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Wandiba amesema maeneo hayo anayoyafanyia kazi kipindi hiki ligi imesimama ni ya kujilinda na la ushambuliaji, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye mechi za timu hiyo zilizopita.

“Balansi yetu kijumla kwa maana ya eneo la kujilinda na ushambuliaji siyo nzuri hadi sasa, hivyo, kipindi hiki tumeona ni vyema kufanyia kazi changamoto hiyo, ili ligi itakaporejea tuwe tumeshaandaa mikakati vizuri,” amesema Wandiba.

Kuhusu mwenendo wa timu hiyo msimu huu, Wandiba amesema anaijua vyema Ligi ya Championship kwa sababu siyo mara yake ya kwanza kufundisha, ingawa, ili watimize malengo ya kukibakisha kikosi hicho msimu ujao anahitaji ushirikiano wa pamoja.

Wandiba aliyewahi kuzifundisha Geita Gold, Pamba Jiji, Mbeya City, Singida United na Alliance FC, alijiunga na timu hiyo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Juma Ikaba kusitishiwa mkataba kwa makubaliano ya pande mbili kutokana na mwenendo mbaya.

Ikaba aliyefundisha timu za Gwasa, Usalama na Baobab Queens, aliiongoza Gunners tangu ikiwa Ligi ya Mkoa (RCL) hadi Championship, ingawa, mwenendo usioridhisha uliwafanya pia mabosi wa kikosi hicho kuusitisha mkataba wake kwa amani.

Gunners ilipanda Championship msimu huu baada ya kuibuka mabingwa wa First League msimu wa 2024-2025, ikiongoza kundi B na pointi 35, pamoja na Hausung kutoka Njombe iliyoongoza ikitokea kundi A na pointi 25.

Katika ligi ya msimu huu, Gunners FC inashika nafasi ya 10 na pointi 23, baada ya kushinda mechi sita tu, sare tano na kupoteza 10, ikifunga mabao 18 na kuruhusu 29.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *