MSHIKE MSHIKE wa Ligi Kuu unaendelea tena leo Jumamosi kwa kushuhudiwa mechi tatu zikipigwa kwenye viwanja mbalimbali, huku mabingwa watetezi Yanga wakiwa na kibarua cha kupambana na maafande wa Tanzania Prisons kuanzia saa 12:30 jioni.

Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam, inazikutanisha timu hizo zikiwa na mwenendo usioridhisha, ambapo Yanga imetoka sare tatu mfululizo na kuweka kibarua cha Kocha, Pedro Goncalves, shakani.

Yanga yenye rekodi ya kucheza mechi 36 za Ligi Kuu bila ya kupoteza, tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 3-1, dhidi ya Tabora United kwa sasa TRA United, Novemba 7, 2024, imekuwa na mwenendo mbaya hali inayotishia kutetea pia taji hilo.

Timu hiyo ilianza kutoka suluhu (0-0), dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC na TRA United, kisha mechi ya mwisho ikatoka sare ya bao 1-1, mbele ya Mtibwa Sugar na kuzidisha presha kubwa kwa Mreno Pedro Goncalves kikosini humo.

Katika mechi hizo 36, ambazo Yanga imecheza kwenye Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza, imeshinda 30 na kutoka sare sita tu, ingawa, msimu huu imecheza 16, ikishinda 11 na kutoa sare tano, ikiendelea kubakia kileleni mwa msimamo na pointi 38.

Kwa upande wa Prisons inayonolewa na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, imekuwa na mwenendo pia usioridhisha, ambapo kikosi hicho cha maafande hakijashinda mechi nne mfululizo, tangu iliposhinda, Februari 14, 2026.

Mechi ya mwisho kwa Prisons kushinda ilikuwa ni ya ushindi wa mabao 3-2, dhidi ya Namungo FC, Februari 14, 2026, ambapo kuanzia hapo, imechapwa mitatu na kutoka sare mmoja, ikiendelea kushika nafasi ya 15, baada ya kukusanya pointi zake 13.

Prisons iliyoanza msimu huu na Kocha, Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno, aliyeondoka Februari 25, 2026, imecheza mechi 17 za Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo kati ya hizo imeshinda tatu, sare nne na kupoteza 10, ikiwa nafasi ya 15 na pointi 13.

Otieno aliyejiunga na Prisons, Julai 24, 2025, kwa msimu wa 2025-2026, aliiongoza timu hiyo ya maafande katika mechi 14, za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo alishinda tatu tu, sare tatu na kupoteza minane, ikifunga mabao manane na kuruhusu 16.

Katika mechi hizo 14, Otieno aliiacha Prisons ikiwa nafasi ya 14 na pointi zake 12, huku Mkenya huyo akizifundisha pia, Gor Mahia FC, Sony Sugar, Posta Rangers na KCB FC zote za kwao Kenya na timu ya taifa ya Kenya maarufu ‘Harambee Stars’.

Kwa upande wa Nsajigwa aliyejiunga na timu hiyo Februari 27, 2026, akitokea Transit Camp inayoshiriki Championship msimu huu, ameiongoza Prisons katika mechi tatu, akiwa hajapata ushindi wowote, baada ya kuchapwa miwili na kutoka sare mmoja.

Mechi ya kwanza kwa timu hizo kukutana, Yanga ilishinda bao 1-0, Machi 12, 2026, lililofungwa na nyota, Laurindo Dilson Maria ‘Depu’ dakika ya 79, huku mara ya mwisho kwa Prisons kuifunga Yanga ilikuwa ni ushindi wa mabao 2-0, Mei 10, 2018.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Matthew Silva, amesema baada ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), wamekuwa na maandalizi mazuri na ya muda mrefu, licha ya kumkosa kipa, Djigui Diarra, aliyefungiwa mechi tatu kwa utomvu wa nidhamu.

“Ni kweli tumepitia kipindi kigumu kwa mechi tatu zilizopita ambazo hatukupata ushindi, tunatambua kiu ya mashabiki zetu ni kuona tunashinda, tunawaheshimu wapinzani wetu, ila tutapambana ili kupata matokeo mazuri,” amesema Matthew Silva.

Kwa upande wa Kocha wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, aliyewahi pia kuichezea Yanga kwa mafanikio makubwa, amesema licha ya ubora wa wapinzani wao, ila wataingia kwa ajili ya kutafuta ushindi, kutokana na kutokuwa sehemu nzuri.

“Hatupo sehemu nzuri na ili tutoke chini tulipo kwa sasa ni lazima tupate matokeo mazuri katika kila mechi tunazocheza, tutacheza kwa nidhamu kubwa ya kujilinda, lakini wakati huohuo tukiwashambulia pia kwa kuwashtukiza,” amesema Nsajigwa.   

MASHUJAA FC V PAMBA JIJI

Kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, wenyeji maafande wa Mashujaa watakuwa na kibarua kigumu cha kulipiza kisasi, wakati watakapoikaribisha Pamba Jiji, katika mechi nyingine kali na ya kusisimua itakayopigwa mapema saa 10:00 jioni.

Katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Oktoba 17, 2025, Mashujaa ilichapwa mabao 2-1, yaliyofungwa yote na Peter Lwasa dakika ya 16 na 64, huku lile la maafande likifungwa na Baraka Mtuwi, dakika ya 45.

Mechi ya mwisho kwa timu hizo kukutana ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Mashujaa ilishinda mabao 2-0, Februari 19, 2025, yaliyofungwa na Hassan Hadji ‘Cheda’ dakika ya 35 na David Ulomi, dakika ya 83.

Mashujaa iliyocheza mechi 17, imeshinda minne tu, sare saba na kupoteza sita, ikiwa nafasi ya 11 na pointi 19, huku kwa upande wa Pamba ikishinda sita, sare saba na kupoteza mitatu kati ya 16, ambapo inashika nafasi ya tano na pointi 25.

NAMUNGO FC V JKT TZ

Mechi ya mwisho kwa leo Jumamosi, itapigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi, kuanzia saa 3:00 usiku, ambapo kikosi cha Namungo FC maarufu ‘Wauaji wa Kusini’, watakuwa na kibarua kingine kigumu cha kuwakaribisha maafande wa JKT Tanzania.

Namungo inayonolewa na Kocha, Juma Mgunda, inaingia katika mechi hiyo ikisaka ushindi wa kwanza, baada ya kikosi hicho kucheza mechi saba mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kushinda, tangu mara ya mwisho iliposhinda, Januari 31, 2026.

Tangu mara ya mwisho ilipoifunga KMC bao 1-0, Januari 31, 2026, Namungo imecheza mechi saba bila ya ushindi, ambapo kati ya hizo imechapwa minne na kutoka sare mitatu tu, ikishika nafasi ya nane, baada ya kukusanya jumla ya pointi zake 21.

Kwa upande wa JKT Tanzania, iko nafasi ya nne na pointi 28, baada ya kikosi hicho cha maafande kushinda mechi saba tu, kikitoka pia sare saba na kupoteza mitatu kati ya 17, ikiwa na rekodi mbalimbali za kuvutia inapokutana na Namungo FC.

Rekodi zinaonyesha, katika mechi nne za Ligi Kuu Bara zilizopita ambazo timu hizo zimekutana hakuna mbabe, huku mara ya mwisho kukutana zilitoka sare ya bao 1-1, Oktoba 19, 2025, ambayo JKT ilikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *